Naibu Waziri akitembelea na kujionea namna ya ufugaji wa Nyuki katika kijiji cha Nyuki Kisaki Manispaa ya Singida.
Meneja wa Shirika la viwanda vidogo vidogo Sido Mkoa wa Singida akisoma taarifa ya Mkoa wa Singinda mbele ya Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe,Exaudi Kigahe.
Naibu Waziri alipata fursa ya kuongea na wafanyabiashara wa mkoa wa Singida ikiwa ni katika kusikiriza na kutatua kero zao.
Singida
Na Mwandishi wetu
Halmashauri zote nchini zimeshauriwa kutenga maeneo maalum kwa ajili ya viwanda na biashara ili kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza sekta ya viwanda vidogo na biashara ndogo.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaudy Kigahe, alipotembelea Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) mkoani Singida akiwa katika ziara yake ya kikazi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kigahe amesema kuwa serikali imeongeza bajeti katika sekta ya kilimo, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda. Hivyo, amezihimiza halmashauri kuhakikisha zinatenga maeneo maalum kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao na biashara ili kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini.
Aidha, Naibu Waziri alipata fursa ya kutembelea wajasiriamali wa SIDO na kujionea bidhaa mbalimbali wanazozalisha. Ametoa wito kwa wadau wa sekta hiyo kuwaunga mkono kwa kuwapatia mafunzo ya kitaalamu na zana za kisasa ili kuzalisha bidhaa zenye ubora na ushindani katika soko la ndani na nje ya nchi.
Katika ziara hiyo, Kigahe pia alitembelea Kijiji cha Nyuki kilichopo Kisaki, Manispaa ya Singida, ambako alishuhudia uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zitokanazo na mazao ya nyuki. Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Philemon Kiemi, ameishukuru serikali kwa kutambua mchango wa viwanda vidogo na kuahidi kuendelea kuzalisha bidhaa bora ili kuchangia uchumi wa taifa.
Ziara yake ilihitimishwa kwa kikao na
wafanyabiashara wa mkoa wa Singida, ambapo walipata fursa ya kuwasilisha
changamoto zao. Miongoni mwa changamoto walizobainisha ni mzigo wa kodi na tozo
mbalimbali, huku wakiiomba serikali kuboresha miundombinu, ikiwemo ujenzi wa
uwanja wa ndege, ili kurahisisha shughuli za biashara na usafirishaji wa bidhaa
kutoka mkoa huo kwenda masoko mengine.
0 Comments