MKURUGENZI WA IKUNGI AKAGUA MAENDELEO YA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA SHULE

 




IKUNGI-SINGIDA

24 Februari 2025 –

 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ndugu Kastori Msigala, akiambatana na wataalam wa halmashauri, ametembelea miradi ya ujenzi wa madarasa na vyoo katika shule za msingi Samaka, Dadu, Kintandaa, na Mnang’ana.

Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za mkurugenzi huyo za kufuatilia maendeleo ya miradi inayotekelezwa ndani ya wilaya. Akiwa katika maeneo husika, alisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya ujenzi, akibainisha kuwa serikali imeshatoa fedha, hivyo kilichobaki ni utekelezaji wa haraka na kwa ufanisi.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Samaka, Ndugu Eliufoo Mandahu, alieleza kuwa kasi ya ujenzi ni ya polepole kutokana na fundi aliyepatikana kupitia mfumo wa NeST kufanya kazi kwa taratibu na kushindwa kuzingatia mkataba unaomtaka kuwa na mafundi wa kutosha. Aliongeza kuwa iwapo mafundi wataongezwa, ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na matundu sita ya vyoo unatarajiwa kukamilika ifikapo 20 Februari 2025. Mradi huo wenye thamani ya shilingi 79,200,000 unatekelezwa kupitia mpango wa BOOST.

Katika Shule ya Msingi Dadu, mkurugenzi alikagua ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa wenye thamani ya shilingi 5,000,000, fedha zikitoka Serikali Kuu. Aidha, katika shule za msingi Kintandaa na Mnang’ana, ujenzi wa madarasa mawili na matundu sita ya vyoo kwa kila shule unaendelea kwa gharama ya shilingi 58,600,000, huku fedha zikitolewa kupitia mpango wa BOOST.

Mkurugenzi Msigala alihimiza wahusika kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili wanafunzi wapate mazingira bora ya kujifunzia.





Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments