Na mwandishi wetu.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Dkt.
Selemani Mwenda, amegawa hatimiliki za kimila 500 na hati za viwanja 5,000 kwa
wakazi wa Kata ya Mbelekese ili kuimarisha umiliki halali wa ardhi na kuzuia
migogoro ya ardhi.
Hatimiliki hizo zimetolewa kwa vijiji
vya Usure, Mbelekese, na Kikonge, zikiwa na lengo la kuondoa migogoro ya
kifamilia hasa wakati wa mirathi au talaka.
Diwani wa Kata ya Mbelekese, Omari
Shabani Wawa, amemshukuru DC Mwenda kwa juhudi hizo na kusisitiza kuwa hatua
hiyo itasaidia sana jamii. Pia, mashirika yasiyo ya kiserikali—Adventus na
Ukijani—yamechangia miti na mbegu kwa ajili ya mazingira na kutoa mizinga 60
yenye thamani ya Sh 9 milioni kwa ajili ya ufugaji wa nyuki.
Zaidi ya kilo 800 za majani kwa lishe
ya mifugo zilitolewa kwa wafugaji, huku wakulima 20 wakipimwa udongo wa
mashamba yao ili kuboresha mazao. Wananchi walijitokeza kwa wingi kupima afya,
ambapo chupa 15 za damu zilichangwa, watu 74 walipimwa afya, na 100 walipimwa
presha na uzito.
Katika sherehe hizo, vikundi vya
akinamama vilileta miche 1,000 ya miti kwa ajili ya biashara, huku wakazi wa
Mbelekese wakihamasishwa kuanzisha ufugaji wa samaki. Wakulima pia
wamehamasishwa kutumia mbolea na mbegu bora ili kuongeza uzalishaji, huku
viwanda vidogo vinne vya mafuta ya alizeti vikichochea kilimo cha zao hilo.
Wananchi wamempongeza Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma za kijamii na maendeleo ya kiuchumi,
wakiahidi kumuunga mkono katika uchaguzi ujao.
0 Comments