MCHIMBAJI MADINI AFARIKI DUNIA SHIMONI



Iramba-Singida

Mchimbaji mmoja wa madini ya zirkoni katika machimbo ya madini hayo yaliiiyoko kijiji cha Kipuma kata ya Nduguti wilaya ya Iramba mkoani Singida Jafari Juma Sukari (42) amekutwa amekufa  juzi  asubuhi akiwa shimoni alipokwenda kuchimba madini hayo usiku akiwa na tochi yake akiwa peke yake.

Akizungumzia hali iliyotokea kwa marehemu kwenye Ibada ya mazishi yake kijijini kwao Sepuka jana Imamu wa msikiti wa Kipuma Juma Ramadhani Jengi amesema tukio hilo lilitokea juzi usiku wakati marehemu alipoondoka kambini saa 5.00 usiku kwenda kuchimba Zirkoni kwenye shu,o lake akiwa na zana zote na tochi yake.Jengi amesema, siku hiyo jioni mvua kubwa ilikuwa imenyesha na ardhi yote ilitota na kwa kuwa ina changarawe  ilikuwa nia rahisi kutumbukia ndani nandio hasa ukuta wa ndani wa shimo hilo ulikatika na kumuangukia marehemu.

Amesema ajali hii imetokea mwenzetu usiku akiwa kazini akitafuta riziki, ameangukiwa na kifusi na sisi tumepata taarifa asubuhi na tulpofika tulikuta kwenye shimo lake viatu na kofia vikiwa nje na huku shimo lake limeziba kwa ndani hapo hapo tukagundua mwenzetu amefukiwa.

Aliendelea kusema” tulipiga mayowe, watu wakafika tukaanza kumfukua tukampata akiwa tayari amekwisha kufa  huku tochi ikiwaka tukagundua kuwa amelala baada ya kuchoka kufanya kazi hapo tukamtoa, tukangoja polisi na walipofika walituambia hiyo ni ajali  ni bahati mbaya mtu kafia kazini kwake nendeni mkamzike”.Alisema.Akitoa hotuba katika mazishi hayo Shaikh Jumanne Mayogho amesema jeneza linaloonekana mbele yetu ni mawaidha tosha kwa mwanadamu kuweza kutafakari maisha yake yaliyobaki kwa sababu kila mtu muda wake ukifika anaondoka.

Mayogho alidokeza kuwa mauti ni adui mkubwa wa wanadamu na viumbe vyote vilivyo hai hutenganisha roho na mwili na mwanadamu akibaki gogo tu, mauti  hutenganisha mtu na familia yake, hutenganisha mtu na mali yake, mauti hayajui mtu alikuwa na kazi nzuri au mcha Mungu na mtu kama hataogopa mauti basi maisha yake yana uwalakini.

Ameendelea kusema Mungu amempa mwanadamu mtihani katika maisha yake,amepewa mali,watoto,neema na shari na akahangaika sana nayo akamsahau muumba wake,akasahau maagizo ya Mungu wake na mwisho akasahau mauti lakini mauti hayasahau mtu na asipokuwa makini atapata taabu duniani  na akhera,Alisema. Katika Ibada hiyo  ya mazishi ya Jafari yalihudhuliwa na ndugu,marafiki,wachimbaji,viongozi wa vijiji,viongozi wa chama na serikali na wachimbaji wenzake walitoa sh.72,000/= kama rambirambi kwa familia ya mwenzao.Mwisho

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments