Na,Jumbe Ismailly MANYONI
KESI ya kuharibu mali pamoja na wizi inayowakabili wakazi watatu wa Tarafa ya Itigi,Wilayani Manyoni,Mkoani Singida inaendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya ya Manyoni.
Shauri hilo la jinai namba 277/2017 lililofunguliwa Mahakamani hapo Sept.28,mwaka jana lipo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo,Bwana Ferdinand Kiwonde.Shahidi wa tatu katika shauri hilo ambaye pia ni mjumbe wa nyumba kumi katika mtaa wa Mlowa Ziginali mjini Itigi, Bwana Emanueli Mika(42) amesema ameanza kuwafahamu washitakiwa hao tangu mwaka 2006 na nyumba yake imepakana na nyumba ya mshitakiwa namba moja Mussa Haruna umbali wa takribani hatua 15.
Mjumbe huyo wa nyumba kumi amesema akiwa nyumbani kwake sept,23,2017 ameshuhudia kundi la watu wakiwa nyumbani kwa Haruna na hivyo kwa kuwa ni kiongozi wa eneo hilo alikwenda mpaka kwenye nyumba hiyo na kukuta watu wamejaa huku gari la polisi likiwa limesimama nje ya nyumba hiyo.
Amebainisha kuwa wakati akiwa nyumbani kwa mshitakiwa huyo ndipo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Itigi, Bwana Pius Luhende alifika katika nyumba hiyo huku akiwa amefuatana na askari na kisha kushuhudia Mussa Haruna akishushwa kwenye gari la Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Itigi.
Kwa mujibu wa shahidi huyo,mshitakiwa huyo ameshushwa kwenye gari hilo pamoja na bomba tatu za chuma na kisha kuanza kupigwa picha na kumpakia kwenye gari pamoja na bomba zake kumpeleka kwenye kituo kikuu cha polisi Manyoni kabla ya kufikishwa Mahakamani hapo.
Kesi hiyo inawahusia watu watatu wakazi wa Mji mdogo wa Itigi,wilayani Manyoni ambao ni pamoja na Mussa Haruna(47)mkazi wa Kijiji cha Mtimkavu,Simon Yohana (42) mkazi wa Kijiji cha Mtimkavu na Joseph Alphonce(69) mkazi wa Kijiji cha Mlowa.Hata hivyo Hakimu aliiahirisha kesi hiyo hadi Machi, 05,mwaka huu Mahakama hiyo itakapoendela kupokea tena ushahidi kwa upande wa utetezi.
Katika hatua nyingine,Mhasibu wa mradi wa maji wa Kijiji cha Londoni,wilayani Manyoni,Vumilia Stephano amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi wilaya ya Manyoni kujibu tuhuma zinazomkabili za wizi wa shilingi 9,800,000/= mali ya serikali ya Kijiji cha Londoni.
Mwendesha Mashtaka wa serikali,Bwana Geofrey Luhanga amedai kwamba mshitakiwa ametenda kosa hilo Nov,01,mwaka 2017 saa nane mchana kwenye eneo la Tawi la Benki ya NMB Manyoni.
Hata hivyo mshtakiwa huyo amekana shitaka hilo na yupo nje hadi Machi,06,2018 kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa.
0 Comments