Mkurugenzi wa Halmashauri ya Hanang BwBryceson Kibassa akisikiliza jambo pembeni ni mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Mh George Bajuta. |
Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang wakimsikiliza mkurugenzi (hayupo kwenye picha) katika mkutano maalum wa baraza la madiwani. |
Na,Jumbe Ismailly
HANANG
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang,Mkoani
Manyara,Bryceson Kibassa amepiga mafuruku walimu wa shule za msingi kuwatoza
wazazi na walezi wa watoto michango ya aina yeyote ile na kuwahakikishia kwamba
hakuna mtoto wa wilaya hiyo atakayetakiwa kukosa elimu kwa kisingizio cha
kutolipa michango.
Akitoa tahadhari hiyo kwenye mkutano maalumu wa Baraza la
madiwani lililokutana kupitisha mapendekezo ya makisio ya mpango na bajeti ya
mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 uliofanyika katika ukumbi wa
mikutano wa Halmashauri hiyo,Bwana Kibassa amesisitiza kwamba kusiwepo na mtoto
yeyote yule wa Hanang ambaye atashindwa kwenda kusoma shule kwa
kisingizio wa mchango wa aina yeyyote ile.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo michango inayoruhusiwa ni ile tu
ya kijamii wanayokubaliana kwa ajili ya kuboresha miundombinu bila kugusa ile
michango ambayo kwenye waraka inatajwa kwamba,isiwe kikwazo cha kuzuia mtoto
yeyote kwenda shuleni.
Hata hivyo Bwana Kibassa amesisitiza kwamba agizo hilo lisije
likatafsiriwa kwamba michango ya miundombinu ambayo inapitishwa katika vikao
halali ya kijamii imezuiliwa,na badala yake kinachozuiwa ni ile michango ambayo
imefafanuliwa vizuri kwenye waraka na endapo hawatakuwa wameuelewa waraka huo
wasisite kuomba ufafanuzi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,Bwana Charles Yona
licha ya kuahidi kwa niaba ya madiwani kutoa ushirikiano kwa watendaji wa
Halmashauri hiyo,lakini ameonyesha kutoridhishwa na hali ya mapato
yaliyopatikana mpaka katika kipindi cha robo ya pili ya kwamba kuwa siyo nzuri
huku kukiwa kuna changamoto lukuki katika kila kata.
Akisoma mapendekezo ya makisio na bajeti ya mapato na matumizi
kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 ya jumla aya shilingi bilioni
38,435,735,692,Ofisa Mipango wa Halmashauri hiyo,Bwana Pantaleo Mkangara
amesema kati ya kiasi hicho cha fedha mapato ya ndani yasiyo na masharti ni
2,493,330,000/= na mapato yenye masharti ambayo ni ruzuku ya matumizi mengineyo
ikiwemo fidia ya vyanzo vilivyofutwa ni 470,172,000/=.
Akifunga mkutano huo maalumu wa baraza,Mwenyekiti wa Halmashauri
hiyo,Bwana Gorege Bajuta amewakumbusha watendaji wa Halmashauri hiyo juu ya
umuhimu wa kupunguza hoja za ukaguzi na kuonya kuwa hawategemei kuona
Halmashauri hiyo ikiendelea kupata hati chafu au hati yenye mashaka,labda tu
kuwepo hoja za nyuma zilizokataliwa kupitishwa.
0 Comments