Katibu wa CCM mkoa wa Singida Jimson Mhagama |
CHAMA Cha Mapinduzi mkoa wa Singida,kimesema kuwa sababu
zilizotolewa na aliyekuwa mbunge wa jimbo la Singida kaskazini Lazaro Nyalandu
zilizosababusha aache ubunge,hazina mashiko,isipokuwa
kilichomsukuma afikie maamuzi hayo,ni hasira za kukosa uwaziri na
si vingenevyo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana
(30/10/2017) Katibu wa CCM mkoa wa Singida,Jamson Mhagama,amesema sababu zote
ikiwemo ya kudai katiba,kimsingi hazina msingi kupelekea mtu kujivua ubunge.
Alisema katika nchi zote jirani,hakuna nchi ina katiba bora na
inayoheshika mbele ya wananchi, kama hii yetu.
“Kwa muono wake ameona siasa za nchi haziendi vizuri na kuamua
kwenda kusaka siasa zitakazompendeza,tunamtakia kila la kheri.Ila tunamwonya
kuwa asitarajie tena kupata ubunge kupitia CHADEMA anakolilia kwenda.CCM
itashinda kwa kishindo katika uchaguzi mdogo ujao”,alisema.
Akisisitiza alisema kwa auamuzi wake,Nyalandu si mwezao tena na
hatapata ushirikiano kwa mwana CCM ye yote.Mwana CCM atakayebainika kuwa karibu
na Nyalandu,atanyang’aywa unachama mara moja.
“Wananchi (wapiga kura) walimwamini Nyalandu katika vipindi
vyote vinne, kwa kumpa kura za kutosha za nafasi ya ubunge.Kupitia kura
hizo,Nyalandu amesifika na kujulikana kila kona.Sasa ameamua kuwapa kisogo
wakazi wa jimbo la Singida kaskazini,jina lake linaenda kufutika na hatasikika
tena”,amesema Mhagama.
Katika hatua nyingine,katibu Mhagama,ametumia fursa hiyo
kuziomba mamlaka zinazohusika,zifanyie uchunguzi wa kina makando kando dhidi ya
Nyalandu, yaliyokuwa yakitamkwa ya kupandisha ndege rasilimali za taifa
zikiwemo twiga na tembo hai,kipindi ni waziri wa mali asili na utalii.
“Binafsi hadi umri huu sijawahi kupanda ndege,lakini
Nyalandu kwa sababu anazozijua yeye,amepandisha ndege wanyama wetu Tembo na
twiga wakiwa hai.Kama hiyo haitoshi,faru John,ametoweka kipindi Nyalandu
akiwa waziri wa mali asili na utalii.Naomba mamlaka husika zifanye uchunguzi na
ikibainika Nyalandu alitumia madaraka vibaya,afikishwe kwenye vyombo vya
sheria”,alisema.
Kwa upande wake mkazi wa Msisi jimbo la Singida kaskazini,Juma
Kindimanda,alisema Nyalandu hajawatendea haki wao kama walipiga kura wake, wa
kipindi cha takribani miaka 20.
“Kwa kura zetu,Nyalandu ameweza kuaminiwa hadi kupewa nyadhifa
za uwaziri katika wizara mbalimbali.Kura hizi hizi zimepelekea jina lake
lijulikane ndani na nje ya Tanzania.Sasa ameamua kutuacha bila hata kutuheshima
kwa kuja kutangazia uamuzi kwenye jimbo lake.Uamuzi huu hauna ustarabu wala heshima
mbele yetu”,alisema Kidimanda.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Singida Bw Wiliamu Mwang'imba |
Kwa upande wake mwenyekiti mpya CCM wilaya ya Singida,Williamu
Mwang’imba,alisema kwa ujumla wilaya yao haina shida na Nyalandu,ameamua
kuondoka,basi aende salama.
“Ameamua kuwaacha wapiga kura wake na wananchi kwa ujumla wa
Singida kasikazini,na wananchi nao watafanya hivyo hivyo kumuacha na atabakia
tu kwenye historia ya wilaya hiyo,ya kuwaacha bila ustarabu watu waliokuwa
wamemwamini kwa vipindi vinne vya ubunge.
Kwa upande wa Chama Cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA) mkoa
wa Singida,kimempongeza Nyalandu kwa uamuzi wake huo,na kwamba milango ipo wazi
kwa yeye kujiunga na chama hicho pinzani.
Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa,Shaban Limu,amesema kwa mujibu wa katiba
yao,wanapokea mtu ye yote kutoka ko kote kuwa mwanachama,na mambo mengine
yataendelea baadaye.
Limu amesema Nyalandu ameonyesha ujasiri na ukomavu kwa
kuweka wazi, kwamba hakubaliani kwa ujumla na mambo mengi ikiwemo siasa
yanavyokwenda hivi sasa nchini.
“Alichofanya Nyalandu,ni sahihi kabisa.Wapo baadhi ya viongozi
wakiwemo mawaziri na wabunge,hawaridhiswi na hali iliyopo hivi sasa,lakini ni
waoga wanaogopa kupoteza maslahi yao, au uwaziri na ubunge wao”,alisema Limu.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa siasa ni sehemu ya maisha na baada
ya siasa,pia yapo maisha na yataendelea kuwepo.
0 Comments