YANGA SC leo imezindua utaratibu wa wanachama
wake kuichangia klabu kupitia simu za mikononi ambao utasimamiwa na kampuni ya
Selcom ya Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa
amesema leo katika mkutano na Waandishi wa Habari mjini Dar es Salaam kwamba
utaratibu huo unaanza mara moja.
Mkwasa ambaye ni mchezaji na kocha wa zamani
wa Yanga, aliitaja namba ya kuchangia kuwa ni 150334 ambayo watumiaji wa
mitandao yote ya simu za mkononi wanaweza kuitumia kuchangia klabu yao.
Mkwasa amesema kwamba wameingia mkataba wa
awali wa majaribio na Selcom kwa miezi mitatu na watakapoona zoezi hilo lina
manufaa kwao, wataongeza mkataba.
“Huu ni mkataba wa awali tu wa majaribio na
tutakapoona zoezi hili linakwenda vizuri, baso tutakaaa chini na wenzetu
kufikiria namna ya kuongeza,”alisema.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Selcom, Gallus Runyeta alisema
kwamba wana matumaini zoezi hilo litafanikiwa sana na Yanga watafutahia.
“Sisi kama Selcom tunafurahi kuingia katika
ndoa hii na Yanga ambayo ni klabu kongwe na wapenzi wengi hapa nchini, na
tunawaomba watu wote wenye mapenzi na Yanga wajitokeze sasa na kuanza
kuichangia klabu yao,”alisema Gallus.
Wakati huo huo: Mkwasa amesema kwamba kikosi
cha Yanga kitaondoka kesho Dar es Salaam kwenda Dodoma kwa mchezo mmoja wa
kirafiki kikiwa njiani kuelekea Mwanza, ambako Jumapili kitakuwa na mchezo wa
mashindano.
Yanga watamenyana na Kombaini ya Majeshi
Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma Jumatano, kabla ya Jumapili kuwa wageni wa Mbao
FC Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza katika Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sporrs Federation (ASFC).
Na mapema Jumatatu kikosi hicho kinatarajiwa
kuendelea Dar es Salaam kuendelea na maandalizi ya mechi zake za viporo za Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
0 Comments