KAMATI ya Katiba Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), imeipokonya Simba ushindi wa mezani waliopewa baada ya kufungwa
na Kagera Sugar 2-1 Aprili 2, mwaka huu Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati
ya Saa 72 iliipa Simba SC ushindi wa mabao matatu na pointi tatu baada ya
kujiridhisha, beki Mohammed Fakhi aliichezea timu ya Kagera Sugar akiwa ana
kadi tatu za njano.
Akizungumza na Waandishi wa
Habari jioni hii ofisi kwake, Uwanja wa Karume, Ilala mjini Dar es Salaam,
Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa amesema kwamba Kamati imegundua makosa kadhaa
katika maamuzi ya Simba kupewa ushindi wa mezani.
Alisema kwanza malalamiko ya Simba hayakuwasilishwa ndani ya wakati kwa
mujibu wa kanuni ya 20 kifungu cha kwanza cha kanuni za Ligi Kuu toleo la mwaka
2006 inayotaka malalamiko yote yawasilishwe kwa maandishi Bodi ya Ligi siyo
zaidi ya saa 72 baada ya mchezo kumalizika kwa mchezo.
Akasema pili malalamiko hayo hayakulipiwa ada kwa mujibu wa kanuni ya 20
kifungu cha nne kinachosema ada ya malalamiko ni Sh. 300,000 na kwamba
malalamiko yatakayowasilishwa bila kulipiwa ada au baada ya muda uliowekwa
hayatasikilizwa.
Sababu ya tatu aliyoitaja Mwesigwa ni kwamba kikao cha Kamati ya
Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72
kilikosa uhalali baada ya kuwashirikisha Wajumbe waalikwa ambao siyo sehemu ya
Kamati hiyo.
“Kwa maana hiyo matokeo ya mchezo kati ya Kagera Sugar na Simba Sports
Club yanabaki kama yalivyokuwa awali, vile vile Katiba Sheria na Hadhi za
Wachezaji inamuagiza Katibu Mkuu wa TFF kuwapeleka katika kamati za kinidhamu
na Maadili baadhi ya watendaji wa bodi ya ligi kwa kutokuwajibika katika nafasi
zao na kuipotosha Kamati ya Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania,
maarufu kama Kamati ya Saa 72,”amesema Mwesigwa.
Kuhusu Fakhi, Mwesigwa kama
alikuwa ana kadi za njano ataitumikia katika mchezo ujao wa timu yake.
0 Comments