Taarifa ya kusikitisha iliyotufikia leo kutokea wilayani Rungwe inasema
mwanasoka wa zamani wa Tanzania Prissons, Yanga na Taifa Stars Godfrey Boni
yupo hospitalini akiwa hana fahamu.
wapendasoka.com imefanya jitihada za kuongea na dada yake Boni aitwaye Neema
Boniface ambae amesema kaka yake alianza kuumwa miezi mitatu iliyopita ugonjwa
ambao mpaka sasa haujajulikana.
"Alikua anaumwa lakini alikua na nguvu zake. Alikua anatoka anaenda
kwenye shughuli zake, wakati mwingine anaenda kuangalia mpira"
Alisema dada huyo.
Neema aliendelea kueleza kwamba wiki mbili zilizopita hali ya Godfrey
Boni ilibadilika na kuwa mbaya zaidi ambapo alikua akilalamika kuishiwa nguvu
na wakati mwingine kupoteza fahamu hali iliyolazimu apelekwe hospitali.
"Tulimleta hospitali ya Makandana, Hospitali ya wilaya ya Rungwe
lakini vipimo havikuonesha ugonjwa wowote ndiyo juzi ikabidi apigwe X Ray ya
kifua na vipimo tumeambiwa vimetoka leo lakini jioni wakati madaktari
wameishaondoka kwa hiyo wamesema watatupatia kesho"
Kwa mujibu wa maelezo ya dada huyo ni kwamba hali ya kaka yake si nzuri
kwa sababu hana fahamu.
wapendasoka.com inawaomba wadau na wapendasoka wote kwa ujumla
kulitazama jambo hili kwa uzito wake ili nyota huyu wa taifa aliyetoa jasho
lake kuipeperusha bendera ya taifa letu aweze kupata msaada wa matibabu na
hatimaye kurejea katika hali yake ya kawaida.
Kwa yeyote mwenye nia njema
ya kumsaidia Godfrey anaweza kuwasiliana na dada yake kwa simu namba 0765 359
290.
0 Comments