Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli ameyataka majeshi yote hapa nchini yajipange kuendana na sera ya
ujenzi wa viwanda kwa kuhakikisha viwanda vya kutengeneza mahitaji yanayoweza
kupatikana hapa nchini
Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo mara baada ya kumuapisha
Jenerali Venance Salvatory Mabeyo kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania
katika hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Ametoa wito kwa uongozi mpya wa Jeshi hilo chini ya Jenerali
Venance Mabeyo kuendeleza juhudi za kuilinda nchi na kuhakikisha viwanda vya
kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa ajili ya majeshi kama vile sare na vifaa,
vinajengwa.
Rais Magufuli amempongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstaafu
Jenerali Davis Mwamunyange kwa kuliongoza jeshi hilo kwa kipindi chote
alichokuwa madarakani na kueleza kuwa watanzania wana imani kubwa na JWTZ.
Kabla ya kuapishwa kushika wadhifa wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi
Tanzania Rais Magufuli amemvalisha Jenerali Venance Salvatory Mabeyo cheo kipya
cha Jenerali alichopandishwa kutoka Luteni Jenerali.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Luteni Jenerali James
Alois Mwakibolwa kuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania
(JWTZ).
Luteni Jenerali James Alois Mwakibolwa amechukua nafasi
iliyoachwa wazi na Jenerali Venance Salvatory Mabeyo ambaye sasa ni Mkuu wa
Majeshi ya Ulinzi Tanzania.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Kamishna Juma Ali
Malewa kuwa Kamishna Jenerali wa Magereza.
Kabla ya kuapishwa kushika wadhifa huo, Mhe. Rais Magufuli
amevalisha Kamishna Juma Ali Malewa cheo kipya cha Kamishna Jenerali.
Kamishna Jenerali Juma Ali Malewa amechukua nafasi iliyoachwa
wazi na Kamishna John Casmir Minja ambaye amestaafu.
Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Mhe. Balozi.
Luteni Jenerali Mstaafu Paul Meela kuwa Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Mhe. Balozi Luteni Jenerali Mstaafu Paul Meela anachukua nafasi
ya Mhe. Balozi Antony Ngereza Cheche ambaye amestaafu.
Pia, Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Mhe. Balozi Samuel
Shelukindo kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa.
Mhe. Balozi Samuel Shelukindo anachukua nafasi iliyoachwa wazi
na Mhe. Balozi Begum Taj ambaye amestaafu.
Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Bw. Nyakimura Mathias Muhoji kuwa
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma.
Bw. Nyakimura Mathias Muhoji anachukua nafasi iliyoachwa wazi na
Claudia Mpangala ambaye amestaafu.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia tukio la
kuapishwa kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kamishna Robert Boazi
Mikomangwa.
Kamishna Robert Boaz Mikomangwa ameapishwa na Mkuu wa Jeshi la
Polisi nchini Inspekta Jenerali wa Polisi - Ernest Mangu.
hafla hiyo imehudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu Mhe. Kassim
Majaliwa, Kaimu Jaji Mkuu Mhe. Prof. Ibrahim Khamis Juma na Mke wa Rais Mama
Janeth Magufuli.
0 Comments