HALMASHAURI ZA WILAYA NA MANISPAA MKOANI SINGIDA KUANZISHA DAWATI LA KUTOA MAELEKEZO MUHIMU



Mkuu wa mkoa wa Singida Dr Rehema nchimbi
MKUU wa mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi ameziagiza halmashauri za wilaya na Manispaa mkoani humo kuanzisha dawati la kuhamasisha na kutoa maelekezo  muhimu kwa sekta binafsi katika kutumia ipasavyo fursa za kiuchumi kufutia makao  makuu ya nchi kuhamia Dodoma.

Dk Nchimbi alitoa agizo hilo kwenye mahojiano maalum na waandishi habari ofisini kwake ambapo, pamoja na mambo mengine, alitakiwa kutaja vipaumbele vyake katika kuharakisha maendeleo kwa wananchi baada ya kuhamishiwa hivi karibuni mkoani  humu  kutokea Njombe.

Alisema kuwa makao makuu ya  nchi kuhamishiwa katika  mkoa  jirani wa Dodoma kunatoa  fursa nyingi za kiuchumi na kijamii kwa njia za uwekezaji kwenye sekta mbalimbali; ikiwemo sekta binafsi.

Kutokana na hali hiyo, alisema  kuna haja kwa kila Halmashauri kuanzisha dawati maalum la  sekta binafsi kwa ajili ya kuhamasisha, kutoa maelekezo na  misaada mingine juu ya namna bora ya kutumia fursa hiyo katika kuibua, kubuni, kuanzisha na kutekeleza miradi ya kiuchumi.

Dk Nchimbi alisema kuwa fursa hizo ni pamoja na  ujenzi wa nyumba  bora na za kisasa  za kulala wageni, Mahoteli, viwanda vikubwa, shughuli za Utalii, usindikaji wa mazao ya kilimo, kilimo cha kisasa na  biashara yenye tija.

Hata hivyo, alisema kuwa hatua hiyo ni lazima iende  pamoja na  kutenga maeneo ya uwekezaji na kuyatangaza kwa wadau sanjari na  kupunguza  urasimu uliopo katika  utoaji wa maeneo hayo ili kuvutia wawekezaji   wengi zaidi. 
Aidha, alitaja vipaumbele mbele vingine kuwa ni kujenga uwanja wa ndege mkubwa na wa kisasa, kuwa na umwagiliaji wa mifugo kwa kuchimba mabwawa ya kutosha na kila kijiji kuwa na ekari 20 za msitu kisiwa. na Abby nkungu Singida

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments