Serikali imevipiga
marufuku Klabu za ligi kuu Tanzania hususani Simba, Yanga na Azam kuwatumia
wachezaji wa kigeni mpaka watakapokamilisha taratibu zao za uhamiaji.
Uamuzi huo umekuja
siku chache baada ya klabu ya Ndanda FC kutuma malalamiko TFF kwamba Simba
iliwatumia wachezaji wake wawili wa kigeni Daniel Agyei na James Kotei kwa
madai kwamba hawana vibali vya kufanya kazi nchini.
Klabu hizo zimepewa
maagizo kwamba wachezaji na makocha wote wa kigeni ambao hawajakamilisha
taratibu za uhamiaji hawatoruhusiwa kuzihudumia klabu zao hadi hapo
watakapokamilisha taratibu hizo.
Idara ya uhamiaji
kupitia kwa afisa uhamiaji John Msumule leo alitoa tamko kwa klabu zote za Ligi
Kuu Tanzania bara kutoendelea kuwatumia wachezaji wake wa kigeni hadi
watakapotimiza masharti ya uwepo wao nchini kisheria na uhamiaji wamezitaka
klabu za Simba, Yanga na Azam FC kuhakikisha wachezaji wake na makocha wao wa
kigeni wanapata vibali vya kufanyia kazi nchini pamoja na kuishi.
Hata hivyo kwa
upande wa Yanga wao wachezaji wao wana vibali vya kazi na vya kuishi nchini
isipokuwa makocha wao ndio wana vibali vya kazi pekee.
Kwa upande wa watani zao wa jadi Simba wao hawajatimiza vigezo
hivyo kwa wachezaji wao wa kigeni na makocha wao, hivyo hawaruhusiwi kuendelea
kuwatumia wachezaji wao ambao hawana vibali mpaka watakapo vipata vibali ingawa
uongozi wa klabu ya Simba ulisema kuwa wachezaji hao wamekamilika kila kitu.
0 Comments