“TAKUKURU SINGIDA YAOKOA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 41 KUPITIA UFUATILIAJI WA MIRADI YA MAENDELEO”


     

                 Onesmo Mdegela akiongea kwa niaba ya Mkuu wa TAKUKURU Mkoa Singida.





 SINGIDA

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida imefanikiwa kuokoa zaidi ya shilingi milioni 41 katika kipindi cha Januari hadi Machi 2025, kupitia ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa mkoani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za TAKUKURU mjini Singida, Bw. Onesmo Mdegela – akimwakilisha Mkuu wa TAKUKURU Mkoa – alisema taasisi hiyo imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa viwango stahiki na fedha za umma zinatumika ipasavyo.

“TAKUKURU ina jukumu la kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya miradi hiyo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa,” alisema Bw. Mdegela.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, jumla ya miradi 25 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 19 ilifuatiliwa katika kipindi husika. Miradi hiyo ilihusisha sekta muhimu kama vile Elimu na Mahakama. Sambamba na hilo, TAKUKURU iliendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya rushwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa.

Katika hatua nyingine, TAKUKURU Singida ilipokea jumla ya malalamiko 99 kutoka kwa wananchi, ambapo 48 kati yake yalihusiana moja kwa moja na vitendo vya rushwa, na 51 yalihusu masuala mengine yasiyohusiana moja kwa moja na rushwa. Taarifa hiyo ilitolewa wakati wa kikao cha kawaida cha kutoa mrejesho kwa vyombo vya habari.

Hatua hizi ni sehemu ya jitihada za taasisi hiyo kuhakikisha uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasilimali za umma, sambamba na kushirikisha wananchi katika mapambano dhidi ya rushwa.

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments