WATAALAMU WA ARDHI SINGIDA WAPATIWA MAFUNZO YA MFUMO WA e-ARDHI.

 

Kamishina Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida Shamimm Hoza akiongea baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika mkoani Singida.



SINGIDA

 Mfumo wa kidijitali wa e-Ardhi unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma za ardhi kwa wananchi wa Mkoa wa Singida, kwa kupunguza misongamano, mizunguko isiyo ya lazima pamoja na muda wa kufuatilia huduma katika ofisi za ardhi.

Kupitia mfumo huo, wananchi wataweza kupata huduma mbalimbali za ardhi kwa njia ya mtandao, hatua inayolenga kuongeza ufanisi, uwazi na urahisi wa upatikanaji wa huduma.

Akizungumza Septemba 14, 2026, mkoani Singida wakati wa mafunzo kuhusu uendeshaji wa mfumo huo na namna wananchi watakavyonufaika nao, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Singida, Bi. Shamim Hoza, amesema e-Ardhi itasaidia kuboresha kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma za ardhi.

Bi. Hoza amesema mfumo huo utapunguza msongamano wa wananchi katika ofisi za ardhi, kuondoa mizunguko isiyo ya lazima katika kufuatilia huduma na kuongeza uwazi katika utoaji wa huduma.

“Mfumo huu utaongeza uwazi na kupunguza msongamano usio wa lazima katika ofisi zetu,” amesema Bi. Hoza.

Aidha, Kamishna Hoza amewataka wataalamu wa ardhi katika Mkoa wa Singida kuupokea mfumo huo na kuhakikisha wanakuwa na uelewa na uwezo wa kuutumia ipasavyo, akieleza kuwa ni hatua muhimu kuelekea utoaji wa huduma bora zaidi kwa wananchi.

Kwa upande wake, Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Ibrahim Magessa, amesema mfumo huo utarahisisha upatikanaji wa huduma za ardhi kwa wananchi, hususan katika kuomba nyaraka mbalimbali ikiwemo hati za umiliki wa ardhi.

Naye Afisa Mipango Miji wa Manispaa ya Singida, Koletha Timanywa, amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa wataalamu wa ardhi kutokana na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Amesema ni jukumu la wataalamu hao kuhakikisha wanaufahamu na kuumudu mfumo wa e-Ardhi ili kuongeza ufanisi na kuboresha zaidi huduma wanazowapatia wananchi.

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments