Rais Dk. John Magufuli, amemteua aliyekuwa Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka kumwakilisha
katika mkutano wa makazi wa Habitat III unaofanyika katika mji wa
Quito, Ecuador.
Taarifa iliyoituma kwenye mitandao ya jamii na Profesa
Tibaijuka jana, ilisema katika msafara huo amefuatana na Katibu
Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Mandeleo ya Makazi, Dk. Yamungu Kayandabila.
“Hivi sasa niko Geneva, Uswisi kwa
matayarisho nikielekea Quito Ecuador mkutano wa makazi duniani wa HABITAT
III kumwakilisha Rais wetu nikiwa pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya
Ardhi,namshukuru Rais kwa heshima hii kubwa, Sitamuangusha.
Habitat III,ni mkutano wa uamuzi na mustakabali wa Shirika
la Makazi Duniani na agenda ya maendeleo endelevu ya miji.
“Kama tunavyojua mkutano wa Habita I
ulifanyika Vancouver,Canada mwaka 1976, Habitat II ulifanyika Istanbul, Uturuki
mwaka 1996 na huu Ecuador Marekani ya Kusini 2016,”alisema.
Alisema kila baada ya miaka 20 wakuu wa nchi hukutana
kukubaliana namna ya kuendeleza makazi kupitia Shirika la UNHABITAT ambalo
aliwahi kuliongoza kwa miaka 10.
“Rais Magufuli alichaguliwa na
kuongoza Baraza la Uongozi wa shirika hilo (Governing Council) kwa muhula wa
mwaka 2006/2008 alipokuwa Waziri wa Ardhi.
“Wafanyakazi walimpenda kiasi kwamba
alipobadilishwa wizara na kupelekwa Mifugo na Uvuvi karibu iwe zogo
ofisini kwangu wakidai tutayumba.
“Niliwatuliza na kuwaambia
kumbadilisha wizara hakumuondolei uenyekiti wake na kweli aliendelea nao na
kumaliza,”alisema Tibaijuka.
Alisema katika mkutano huo, jambo kubwa atakalolipigania ni
utaratibu wa shirika hilo kuzisaidia nchi zinazoendelea kama sisi kwa
kuzikopesha halmashauri zao fedha za miundombinu, bila kuilazimisha Serikali
kuu kutoa dhamana kwa mikopo hiyo.
Alisema jambo hilo ni la msingi kwa vile
huleta kasi ya maendeleo ingawa huwa linapingwa na wakubwa wanaotaka
kukopa kupitia Serikali kuu ili waibane kwa kutumia Benki ya Dunia,
kitendo ambacho kinachelewesha kasi ya maendeleo.
“Tutajitahidi
kulingana na maelekezo ya Rais tunayemwakilisha kuhusu msimamo wa nchi yetu na
washirika wake ambao ni nchi za Afrika na za G77 na China,” alisema.
0 Comments