Afisa mahusiano wa Shirika la TANESCO Mkoa wa Singida Ibrahim Solo akitoa Elimu juu ya matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia katika Semina ya Viongozi wa Dini Mjini Singida.
SINGIDA
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa
Singida limeongeza kasi ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya Nishati
Safi ya Kupikia, likilenga kuwafikia wananchi kuanzia ngazi ya Kata hadi
Vijiji.
Katika
kuendeleza juhudi hizo, TANESCO Singida limeendelea kutoa elimu kuhusu matumizi
ya majiko ya umeme yanayojulikana kama “Jiko Janja”, ambayo yanapatikana kwa
gharama nafuu na kutoa fursa kwa wananchi kutumia nishati safi na salama katika
shughuli zao za kila siku.
Elimu hiyo
imekuwa ikitolewa kwa makundi mbalimbali katika jamii, yakiwemo taasisi na
jumuiya za kidini, kwa lengo la kuongeza uelewa na kuhamasisha matumizi ya
nishati safi ya kupikia.
Katika hatua
hiyo, TANESCO Mkoa wa Singida imetoa elimu kwa walimu wa Madrasa pamoja na
wawakilishi wa taasisi na jumuiya zilizopo chini ya Bakwata Mkoa wa Singida,
ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha ujumbe kuhusu matumizi ya nishati
safi unawafikia wananchi wengi zaidi.
Akizungumza
wakati wa semina hiyo, Afisa Mahusiano wa TANESCO Mkoa wa Singida, Ibrahim
Solo, amewataka wananchi kutumia fursa ya kupata majiko ya umeme aina ya “Jiko
Janja”, ambayo yanapatikana katika ofisi za TANESCO.
Solo amesema
matumizi ya “Jiko Janja” yana unafuu zaidi katika matumizi ya nyumbani, huku
akisisitiza kuwa jiko hilo lina kiwango kizuri cha usalama kwa matumizi ya
familia.
“Tunawahamasisha wananchi kutumia majiko ya ‘Jiko Janja’ ambayo yanapatikana katika ofisi za TANESCO. Matumizi yake yana unafuu zaidi na yana usalama mkubwa kwa matumizi ya nyumbani,” amesema Solo.
Amesema
matumizi ya majiko ya umeme yanaweza kuwa chaguo muhimu kwa familia zinazotaka
kutumia nishati safi katika kupikia, huku wananchi wakitakiwa kupata elimu
sahihi kuhusu matumizi salama na yenye ufanisi ya vifaa hivyo.
Kwa upande
mwingine, kuendelea kwa elimu hiyo kunalenga kuwapa wananchi uelewa mpana
kuhusu umuhimu wa nishati safi ya kupikia, ikiwemo faida zake katika kuboresha
mazingira ya nyumbani na kupunguza utegemezi wa baadhi ya nishati zinazozalisha
moshi.
Elimu hiyo
pia inatoa fursa kwa wananchi kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kuhusu
matumizi sahihi ya majiko ya umeme, gharama zake pamoja na namna ya kuyatumia
kwa usalama.
Semina hiyo
ya walimu wa Madrasa pamoja na wawakilishi wa taasisi na jumuiya zilizopo chini
ya Bakwata Mkoa wa Singida imeandaliwa na Jumuiya ya Kuhifadhi Qur’an Tanzania,
kwa kushirikiana na Ofisi ya Bakwata Mkoa wa Singida.
Semina hiyo
imefanyika katika Ukumbi wa Bakwata Wilaya ya Singida, ikiwa ni sehemu ya
juhudi za kuunganisha nguvu kati ya taasisi mbalimbali katika kuelimisha jamii
kuhusu matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.
TANESCO Mkoa
wa Singida inaendelea kutoa elimu katika maeneo mbalimbali, huku ikihamasisha
wananchi kuchangamkia matumizi ya nishati safi na teknolojia za kisasa za
kupikia kwa ajili ya usalama, ufanisi na ustawi wa familia.






0 Comments