WANANCHI WANUFAIKE NA HUDUMA BORA ZA HARAKA NA UWAZI ZAIDI -RC DENDEGO

 


Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe Halima Dendego akifungua semina ya wataalamu wa Ardhi kutoka katika Halmashauri za mkoa huu.

                              
                                


                             

Singida.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza kutoa mafunzo kwa wataalamu wa sekta ya ardhi mkoani Singida kuhusu matumizi ya mfumo wa kidijitali wa e-Ardhi, hatua inayolenga kuongeza kasi, ufanisi na uwazi katika utoaji wa huduma za ardhi kwa wananchi.

Mafunzo hayo yamefunguliwa leo, Septemba 14, 2026, na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Omary Dendego, ambaye amesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika kuboresha utoaji wa huduma za umma.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Dendego amesema matumizi sahihi ya mifumo ya kidijitali yana nafasi kubwa katika kupunguza changamoto za urasimu, kuongeza uwazi na kuimarisha ufanisi katika usimamizi wa masuala ya ardhi.

Amesema ni muhimu kwa wataalamu wanaoshiriki mafunzo hayo kuhakikisha wanatumia kikamilifu maarifa wanayopata, ili mfumo wa e-Ardhi uweze kutimiza malengo yake na hatimaye kuwawezesha wananchi kupata huduma bora, za haraka na zenye uwazi.

“Ni muhimu kutumia fursa hii ya mafunzo kwa ufanisi na kuhakikisha mfumo huu unatumika ipasavyo ili wananchi wanufaike na huduma bora, za haraka na zenye uwazi zaidi,” amesema Mhe. Dendego.

Mafunzo hayo yanawahusisha wataalamu mbalimbali wa sekta ya ardhi, wakiwemo Maafisa Mipango Miji, Wapima, Maafisa Ardhi, Wasajili wa Hati pamoja na Wathamini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha matumizi ya teknolojia katika usimamizi na utoaji wa huduma za ardhi.

Mfumo wa e-Ardhi unalenga kuwezesha huduma mbalimbali za ardhi kutolewa kwa njia ya kidijitali, ikiwemo uwasilishaji na ufuatiliaji wa maombi, usimamizi wa taarifa za ardhi na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Kwa kutumia mfumo huo, Serikali inalenga kupunguza utegemezi wa taratibu za kawaida zinazoweza kuchangia ucheleweshaji wa huduma, huku ikiongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa ardhi.

Hatua hiyo inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuboresha huduma za ardhi mkoani Singida na kuwasaidia wananchi kupata huduma kwa urahisi, haraka na kwa uwazi zaidi, sambamba na kuendana na jitihada za Serikali za kuhamishia huduma zake katika mifumo ya kidijitali.







Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments