TANESCO SINGIDA YAZINDUA “PROJECT MAPATO” KUWAFIKISHIA VIWANDA UMEME MAALUMU


Mhandisi Freank Mlay akiongea na wanahabari katika zoezi la wekaji Nguzo za zege katika mradi wa PROJECT MAPATO unaoendelea sasa katika eneo la Jovena kata ya Mandewa Manispaa ya Singida.



Mashine hii imekuwa mkombozi katika matumizi ya nguvu kazi ya uwekaji wa nguzo za zege hasa katika maeneo yenye changamoto ya maji.

Mafundi wakitumia mashine maalum ya kuinulia nguzo ya zege katika eneo lenye changamoto ya tope.







 

SINGIDA

Na Cales katemana

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida limeanza kutekeleza mradi maalumu wa ujenzi wa njia ya umeme kwa ajili ya wateja wakubwa, hususan viwanda, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuongeza mapato ya shirika huku likiboresha upatikanaji wa huduma kwa kundi hilo la wateja.

Mradi huo unaojulikana kama “PROJECT MAPATO” unatekelezwa katika eneo la Jovena, Manispaa ya Singida, ambapo unahusisha ujenzi wa njia ya usambazaji wa umeme pamoja na uwekaji wa nguzo za zege. 

Kwa mujibu wa TANESCO, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika ndani ya mwezi Septemba 2026.

Akizungumza na wanahabari katika eneo la mradi,Jovena kata ya Mandewa Manispaa ya Singida Mhandisi wa TANESCO Mkoa wa Singida, Frank Mlay, amesema mradi huo unalenga kukidhi mahitaji ya wateja wakubwa na kuchangia katika kuongeza ufanisi wa huduma za umeme.

Mlay amesema moja ya changamoto iliyojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi ni hali ya baadhi ya maeneo kutokuwa na miundombinu mizuri ya barabara, jambo lililosababisha ugumu katika usafirishaji wa nguzo za zege kwenda kwenye maeneo yanayohitajika.

Hata hivyo, amesema TANESCO haikusimama kutokana na changamoto hiyo, badala yake wataalamu wa shirika walibuni na kutengeneza mashine maalumu ya kubeba nguzo, hatua iliyosaidia kurahisisha usafirishaji na kuwezesha kazi za mradi kuendelea kwa ufanisi.

Ubunifu huo umeelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada za TANESCO kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa miradi ya umeme, hasa katika maeneo yenye miundombinu hafifu ya barabara.

Mradi wa PROJECT MAPATO unatarajiwa kuwa na umuhimu kwa maendeleo ya shughuli za viwanda na biashara katika eneo la Singida, kwa kuweka miundombinu maalumu ya umeme inayolenga kuwahudumia wateja wakubwa kwa ufanisi zaidi.

TANESCO Mkoa wa Singida inaendelea na hatua za mwisho za utekelezaji wa mradi huo, huku ikilenga kuukamilisha ifikapo Septemba 2026.

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments