Mshambuliaji wa Stand United ya Shinyanga Abasirim Chidiebere
huenda asizungumze kwa zaidi ya wiki mbili kutokana na nyaya maalum alizofungwa
kwenye taya zake na meno ili kumsaidia kupona majeraha aliyopata wakati
akiitumikia timu yake dhidi Azam FC ikiwa ni mchezo wa ligi kuu Tanznia bara
uliochezwa kwenye uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga.
Daktari wa Stand United amethibitisha kwamba, Chidiebere
hatoweza kufungua mdomo wake katika kipindi chote ambacho nyaya zitakuwa
hazijatolewa kwenye taya kitu ambacho kitamfanya asiweze kula kwa njia ya
kawaida hivyo kutumia mrija maalum utakaomwezesha kula vyakula laini.
Majeraha aliyoyapata Chidiebere yalitokana na kuchezewa vibaya
na beki wa Azam Agrey Morris kwenye mchezo ambao ulimalizika kwa Stand United
kuibuka na ushindi wa bao 1-0, daktari wa Stand United Alphayo Peneheli
ameeleza ukubwa majeraha aliyoyapata mchezaji huyo na muda ambao huenda
akakosekana uwanjani.
“Kilichotokea, mchezaji wa Azam Agrey Morris alimchezea rafu
mchezaji wetu Abasirim Chidiebere alimpiga taya, tuligundua muda huohuo
kilichotokea kwamba aliumia sana tukampatia huduma ya kwanza hapohapo alikuwa
anatokwa damu mdomoni tukamsaidia na badae akakimbizwa hospitali kwa gari la
wagonjwa lililokuwepo uwanjani,” amesema Dr. Peneheli .
“Alipofika hospitali wakagundua kwamba amevunjika taya
wakamtafuta daktari wa meno na kinywa akaona amevunjika taya la chini upande wa
kushoto na kulia, zaidi ameumia upande wa kushoto kwahiyo muda huohuo akapatiwa
huduma, wamemfunga waya juu ya meno na chini ya meno kwa nyaya za kitabibu.
Zinafungwa kiasi kwamba hawezi kufungua mdomo ili kuruhusu mpasuko huo upone.”
“Kawaida tunategemea mpasuko huo utapona kwa wiki sita, wakati
huohuo alikuwa ametoka meno mawili, kwahiyo hapo mdomoni kuna njia ambayo
itamuwezesha kulishwa vyakula laini kama supu ya dagaa, supu ya samaki ambazo
zinakuwa na calcium nyingi, atapata juice ya asili na uji wa mtama au uwele
ambao utaweza kupita kwenye mrija.”
“Anaendelea vizuri baada ya wiki mbili au tatu anaweza
akaondolewa hizo nyaya lakini kwa kupitia kwa daktari wa kinywa na meno baada
ya kuona inafaa. Tunategemea wiki sita hadi saba mpasuko utakuwa umeweza
kupona.
0 Comments