SERIKALI YAENDELEA KUWEKEZA KATIKA MIUNDOMBINU YA ELIMU

 





Arusha

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Februari 23, 2026 amezindua Shule ya Sekondari Sinya iliyopo Kata ya Sinya, Kijiji cha Leremeta, Wilaya ya Longido mkoani Arusha, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu nchini.

Shule hiyo imejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.2 zilizotokana na Serikali Kuu, Mradi wa SEQUIP, TASAF pamoja na mapato ya ndani ya Halmashauri, huku wananchi wakichangia shilingi milioni 34 kusaidia kukamilika kwa ujenzi wake.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt. Nchemba amesema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata mazingira bora ya kujifunzia, sambamba na kupunguza changamoto ya umbali na msongamano wa wanafunzi katika shule zilizopo.

Amesema kukamilika kwa Shule ya Sekondari Sinya kutasaidia kuongeza nafasi za elimu ya sekondari kwa wanafunzi wa Kata ya Sinya na maeneo jirani, na hivyo kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Wilaya ya Longido.

Aidha, Waziri Mkuu amewahimiza wanafunzi kusoma kwa bidii ili kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwemo programu ya ufadhili wa masomo ya Samia Scholarship.

Uzinduzi wa shule hiyo ni kielelezo cha hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kuhakikisha elimu inabaki kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa.

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments