Mashambulizi ya
makombora yamepiga katika kambi ya jeshi la Syria leo (09.04.2018) lakini
Marekani na Ufaransa zinakanusha kuhusika kama hatua ya kujibu shambulizi la
gesi ya sumu lililofanywa Jumamosi mjini Douma.
Shirika la habari la
serikali ya Syria SANA limeripoti mapema leo alfajiri kwamba makombora kadhaa
yamevurumishwa katika kambi ya jeshi ya Tiyas katika mkoa wa kati wa Homs.
Shirika hilo limesema mifumo ya ulinzi wa anga imeanza kutumika na awali
liliripoti kuhusu shambulizi linaloshukiwa kufanywa na Marekani, lakini baadaye
likafuta kabisa kuitaja Marekani.
Shirika
linalofuatilia masuala ya haki za binadamu la Syria limesema wapiganaji 14
wameuawa, wakiwemo wanajeshi wa Iran wanaouunga mkono utawala wa rais wa Syria,
Bashar al Assad.
Msemaji wa wizara ya
ulinzi ya Marekani, Pentagon, amekanusha madai ya Marekani kuhusika na
shambulizi hilo, lakini akasema wanaendelea kuifuatilia kwa karibu hali nchini
Syria na itaendelea kusaidia juhudi za kidiplomasia zinazofanywa kuwawajibisha
waliohusika na shambulizi la sumu katika mji uliozingirwa wa Douma huko Ghouta
Mashariki, siku ya Jumamosi ambapo watu 40 waliuawa.
Rais
wa Marekani, Donald Trump, na mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron, hapo jana
walilaani vikali shambulizi hilo la sumu na kuapa kuchukua hatua za pamoja
kujibu shambulizi hilo ambalo limeibua wasiwasi kote ulimwenguni na kukosolewa
vikali. Trump alisema rais wa Urusi, Vladimir Putin, Urusi na Iran wanahusika
aktika kumuunga mkono mnyama Bashar al Assad na akaonya watalipa kwa gharama
kubwa.
Kiongozi
wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis amesema hakuna kinachoweza
kulihalalisha shambulizi la sumu nchini Syria wakati alipokuwa akiifunga misa
jana Jumapili. Alizungumzia taarifa za kutisha za watu kuuliwa katika
mashambulizi ya mabomu yanayosababisha majeruhi wengi, miongoni mwao watoto na
wanawake.
Rais
wa Uturuki Recep Tayaip Erdogan amelilaani vikali shambulizi hilo la sumu huko
Douma akizituhumu nchi za Magharibi kwa kuupuzilia mbali siasa chafu za kinyama
zinazoendeshwa na utawala wa Syria. Akizunguza mjini Siirt, Erdogan alisema
umma wa Uturuki haukubaliani kabisa na mwenendo huo.
"Tunapinga
kwa nguvu zote undumakuwili huu na siasa hizi za kinyama. Nchi za Magharibi! Ni
lini mtakapogeuka na kuwatazama watoto hawa, wanawake hawa wanaouliwa Ghouta
Mashariki ili tuseme mnatenda haki?"
Baraza
la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana leo kuijadili hali nchini
Syria huku Umoja wa Ulaya ukisema ushahidi wote wa shambulizi la sumu
unaashiria limefanywa na utawala wa Syria. Iran kwa upande wake imesema
shambulizi hilo linatumiwa kama kisingio cha kufanya harakati ya kijeshi Syria.
China
imesema leo inaunga mkono uchunguzi kuhusiana na shambulizi linaloshukiwa kuwa
la sumu mjini Douma huku ikitoa wito kwa baraza la usalama na shirika la
kimataifa la kudhibiti silaha za sumu OPCW kuendelea na jukumu lao kama wadau
wakuu wa kulishughulikia tatizo hilo.
0 Comments