Mbunge wa Jimbo la Singida mjini Mhe, Musa Sima wa kwanza kulia na wapili ni Diwani wa kata ya Utemini Mhe, Kawawa Munjori akifuatiwa na katibu wa Mkoa na makatibu wa Jumuiya ya Wazazi,Wanawake na UVCCM wilaya.
Na Mwandishi Wetu
Wenyeviti na wajumbe wateule wa
Serikali za Mitaa katika Manispaa ya Singida wameapishwa rasmi kuanza
kutekeleza majukumu yao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo
Utemini, Ferdinand Njau.
Katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa
Manispaa ya Singida, Joanfaith Kataraia, aliwataka viongozi hao kuhakikisha
wanawatumikia wananchi kwa uadilifu na kufuata taratibu na sheria za nchi.
Aidha, aliwasisitiza kutatua migogoro bila upendeleo, huku wakizingatia weledi
katika utendaji wao wa kazi.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Wilaya ya Singida Mjini, Naomi Devid, aliwataka viongozi hao kufanya kazi kwa ushirikiano na kuepuka vitendo vya rushwa ambavyo huathiri ufanisi wa kazi na kuharibu taswira ya uongozi. Alisisitiza umuhimu wa kufuata maadili na taratibu za utumishi wa umma.
Baadhi ya wenyeviti na wajumbe
walioapishwa waliahidi kufanya kazi kwa umoja na kuzingatia weledi, huku
wakiwatoa hofu wananchi kuhusu usimamizi wa mali na nyaraka za serikali,
zikiwemo mihuri ya ofisi.
Wito kwa viongozi hao ni kuhakikisha
kuwa wanakuwa kiungo thabiti kati ya serikali na wananchi kwa kusikiliza na
kutatua changamoto za jamii kwa uwazi na haki.
0 Comments