Hizi ni picha mbalimbali zilizochukuliwa wakati wa kikao kilichoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, akizungumza na viongozi wa vyama vya siasa. Kikao hiki kililenga kuhimiza amani, mshikamano, na utulivu kuelekea kufungwa kwa kampeni za uchaguzi wa ngazi ya Serikali za Mitaa.
Singida
Mkuu wa Mkoa
wa Singida, Mhe. Halima Dendego, amekutana na viongozi wa vyama vyote vya siasa
vilivyopo mkoani Singida kwa lengo la kusisitiza umoja, amani, na utulivu
kuelekea uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024. Kikao hicho,
kilichofanyika leo asubuhi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, kimejumuisha
wawakilishi kutoka vyama mbalimbali vya siasa kama CHADEMA, CUF, Demokrasia
Makini, UMD, CCM, NLD, NRA, ACT-Wazalendo, UDP, na CHAUMA.
Akizungumza
katika kikao hicho, Mhe. Dendego aliwapongeza wajumbe wa vyama vya siasa kwa
kufanya kampeni za amani na kuhimiza kuendeleza utulivu uliopo hadi siku ya
uchaguzi na hata baada ya uchaguzi.
"Sisi
sote ni ndugu. Uchaguzi wa Tanzania ni wa Singida pia, na amani ya Tanzania ni
ya Singida. Tuweke tofauti za vyama na dini pembeni. Serikali imekamilisha
taratibu zote, hivyo tarehe 27 ninaomba tuendeleze amani na kuwaunga mkono
watakaochaguliwa," alisema RC Dendego.
Aidha,
alihakikisha usalama wa kutosha wakati wa kampeni, uchaguzi, na baada ya
uchaguzi. Alisisitiza umuhimu wa kutumia siasa za ushindani kwa njia ya sera
badala ya vurugu, akisema ni msingi bora wa maandalizi ya uchaguzi mkuu wa
mwaka 2025.
"Tushindane
kwa sera na mipango, si kwa vurugu. Tuijenge amani mwaka huu kwa msingi bora wa
uchaguzi wa mwaka 2025," aliongeza.
Naye
Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Singida, Hamis Labia, alielezea furaha yake
kwa kuwa na nafasi ya kukutana na viongozi wa vyama vingine, akisema hatua hiyo
ni muhimu kwa kujenga urafiki na mshikamano, pamoja na kujadili changamoto kwa
pamoja.
Kwa upande
wake, Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Singida, Samweli G. Malo, alisisitiza umuhimu
wa uchaguzi wa haki na uwazi kwa kushindana kwa misingi ya kiitikadi na kisera.
Alitoa wito wa kuimarisha ulinzi wa kura na kusisitiza uaminifu kwa mawakala wa
vyama. Pia, alibainisha kuwa CHADEMA imeweka wagombea 3,240 katika vijiji 217
kati ya vijiji 442 vya mkoa wa Singida.
Mwenezi wa
CCM Mkoa wa Singida alielezea kuridhishwa kwake na hali ya utulivu ya uchaguzi
mwaka huu, akibainisha kuwa kampeni zimeendeshwa kwa amani na wagombea wamekuwa
wakinadi sera zao kwa utulivu wa hali ya juu.
Kikao hiki
kimeacha ujumbe mzito wa mshikamano na kuimarisha amani mkoani Singida wakati
huu wa uchaguzi.
0 Comments