Dc Gondwe akifunga Mkutano Mkuu wa Bakwata Mkoa wa Singida kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego.
Katibu wa Bakwata Mkoa wa Singida Ustadh Ommary Muna akiongea katika uchaguzi huo.
SINGIDA
Na Cales katemana
Viongozi wateule wa Baraza la Waislam (BAKWATA) Mkoa wa
Singida wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya katiba na
kanuni za baraza hilo, ili kuimarisha umoja, nidhamu na uadilifu katika uongozi
wa dini.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima
Dendego, wakati akihitimisha uchaguzi wa viongozi wa BAKWATA ngazi ya mkoa,
uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya
Singida, Mhe. Godwin Gondwe, amesema kuwa BAKWATA ni taasisi muhimu inayopaswa
kuwa kioo cha waumini wa dini ya Kiislam, hivyo viongozi wapya wanapaswa
kufanya kazi kwa bidii, uadilifu, na kuzingatia malengo ya baraza hilo.
“BAKWATA ni kioo cha jamii ya Kiislam, hivyo viongozi
mnapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika utendaji, mshikamano na maadili,” alisema
Gondwe.
Aidha, Mhe. Gondwe amewahakikishia viongozi wapya kuwa
Serikali ya Mkoa wa Singida chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa Mhe. Halima
Dendego, itaendelea kushirikiana nao sambamba na taasisi zote za kidini bila
ubaguzi wa imani.
Katika hatua nyingine, akizungumzia suala la amani ya nchi, Mhe.
Gondwe amewataka viongozi wa dini kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha
amani, hususan katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa
kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
“Ni muhimu viongozi wa dini kuwa mstari wa mbele katika
kudumisha amani na kuhamasisha waumini kujitokeza kupiga kura kwa amani na
utulivu,” alisisitiza.
Uchaguzi huo wa BAKWATA Mkoa wa Singida ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na serikali, na ulilenga kuweka safu mpya ya uongozi itakayotekeleza majukumu kwa mujibu wa katiba ya baraza hilo.










0 Comments