Mkurugenzi Mtendaji Halmshauri ya Wilaya ya Ikungi Justice Kijazi (Picha kutoka maktaba yetu)
Na Mwandishi wetu
Halmashauri
ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida imepanga kujenga shule nne za vidato vya
tano na sita pamoja na chuo kimoja cha ufundi (VETA) katika mwaka wa fedha
2024/2025. Hatua hii inalenga kuwawezesha wanafunzi wote wanaofaulu masomo ya
sekondari kuendelea na masomo yao, huku wale wa shule za msingi wakipata
mafunzo ya ufundi ili kuwa na ujuzi wa kujiajiri baadae.
Afisa
Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Dkt. Ngwano John, alieleza hayo katika mahafali ya 24 ya Shule ya Sekondari Sepuka, ambapo
wanafunzi 48 walihitimu kidato cha nne. Dkt. Ngwano alieleza kuwa Serikali ya
Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha
nyingi kwenye elimu nchini, ikilenga kuwawezesha watoto wote kupata elimu na
kushiriki katika maendeleo ya kiuchumi kupitia fursa zilizopo.
Halmashauri
imepanga kujenga madarasa mapya na kukarabati majengo chakavu katika shule za
msingi na sekondari. Aidha, shule nne—Kintandaa, Sepuka, Unyahati, na
Nkuhizitajengewa majengo ya kisasa kwa ajili ya vidato vya tano na sita, huku
chuo cha ufundi kikiwa Utaho.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Ikungi, Justice Kijazi, alifafanua kuwa Wizara ya
Elimu itajenga majengo nane ya kisasa ya madarasa kwa vidato vya tano na sita
katika shule hizo. Majengo mengine kama vile ya utawala, mabweni, mabwalo,
maktaba, na nyumba za walimu pia yatajengwa. Ujenzi huu utagharimu takriban
shilingi bilioni 2.7, ikijumuisha chuo cha ufundi, ili kuhakikisha kuwa
wanafunzi wa Ikungi wanapata elimu bora kwa mujibu wa maelekezo ya Rais Samia.
Mkuu
wa Shule ya Sekondari Sepuka, Deogratus Makene, alisema kuwa shule yake ina
jumla ya wanafunzi 371 na walimu 15. Shule hiyo ina madarasa 12, maabara, jengo
la utawala, na bweni, lakini inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vifaa vya
TEHAMA. Aidha, Makene alieleza kuwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne 2023
hayakuwa mazuri, lakini wana matarajio ya matokeo bora zaidi mwaka huu kutokana
na juhudi za walimu na wanafunzi.
Afisa
Mtendaji wa Kata ya Sepuka, Bahati Mkungile, alieleza kuwa walimu wamejitahidi
kuboresha ufaulu wa wanafunzi kwa kushirikiana na wazazi. Katika kusaidia
masomo ya TEHAMA, wazazi, walimu, na wanafunzi walichanga shilingi milioni 2.134
kwa ajili ya kununua kompyuta, huku walimu wa masomo hayo wakiwa tayari kwa
ajili ya kufundisha mwakani.
0 Comments