Afisa uchunguzi kiongozi msaidizi Takukuru Mkoa wa Singida na akiongea na wakuu wa taasisi mbalimbali binafsi zisizo za kiserikali mjini Singida..
SINGIDA
Na Mwandishi wetu
Jamii imeaswa kuepukana na vitendo vya rushwa hasa katika
kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu hapo
mwakani ili kuchagua viongozi wanaofaa na watakao isaidia jamii na Taifa kwa
ujumla.
Hayo yamesemwa na Afisa uchunguzi kiongozi msaidizi kutoka
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU Mkoa wa Singida Onesmo
Mdegela wakati wa jukwaa la mwaka la mashirika yasiyo ya kiserikali Mkoa wa
Singida lililofanyika katika ukumbi wa RC Mission mjini hapo.
Amesema wananchi wanatakiwa kuwa makini na kuepuka kupokea pesa
au zawadi zingine kutoka kwa wagombea kwani zitawafanya washindwe kufanya
maamuzi sahihi ya kuchagua viongozi watakaowafaa.
Anasema baadhi ya wagombea ambao hawana sifa za kuongoza watu
wamekuwa wakitoa vitu mbalimbali kwa jamii au mtu mmoja mmoja ili kuwashawishi
wananchi wawachague wakati wa uchaguzi ambapo baada ya kuchaguliwa hutumia
nafasi hiyo kurudisha fedha alizogawa bila kujali changamoto za jamii.
Ametumia nafasi hiyo kuwasihi wananchi kutoa taarifa pale
wanapohisi kuna vitendo vyovyote vinaendelea katika jamii vya kutoa au kupokea
rushwa ili kulinda haki ya kila mwananchi na jamii yote.
0 Comments