SERIKALI YAREJESHA UTARATIBU WA HATI PUNGUZO


Serikali imerudisha utaratibu wa kugawa vyandarua vyenye viuatilifu kwa akina mama wajawazito na watoto ambao wanapatiwa chanjo ya surua kupitia vituo vya kutolea huduma za afya ya uzazi na mtoto ambapo utaratibu huo utaanza rasmi mwezi Agosti mwaka huu.

Afisa Muuguzi kutoka Wizara ya Afya Epifania Malingumu amewaambia wajumbe wa mkutano wa uelimishaji juu ya mpango endelevu wa ugawaji vyandarau vyenye viuatilifu vya mda mrefu kuwa kwa sasa vyandarua hivyo havitapatikana katika maduka kama ilivyokuwa kwenye utaratibu wa ‘hati punguzo’ ya zamani.

Malingumu amesema hapo awali vyandarua vyenye viuatilifu vilikuwa vikitolewa kwa mfumo wa hati punguzo ambapo mama mjamzito alikuwa anatakiwa kutafuta maduka ya mawakala wa vyandarua hivyo mara baada ya kupatiwa hati hiyo katika vituo vya kutolea huduma ya afya ya uzazi.

“Utaratibu wa hati punguzo wa zamani ulikwisha muda wake mwaka 2014, akina mama walikuwa wanapata changamoto katika kutafuta mawakala wa vyandarua lakini utaratibu mpya ni kwamba mama mjamzito au mwenye mtoto mchanga atapewa chandarua chenye viuatilifu palepale atakapokuwa katika vituo vya kutolea huduma za afya ya uzazi” amesema.

Ameongeza kuwa mama atapewa chandarua katika hudhurio la kwanza la kliniki ambapo takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 98 ya wajawazito huhudhuria kliniki angalau mara moja pia vyandarua hivyo vitatolewa kwa idadi ya watoto ambao mama atakua amejifungua kwa wakati huo.

Kwa upande wake Mratibu wa zoezi la ugawaji vyandarua nchini Yusufu Mwita amesema vyandarua vyenye viuatilifu ni nyenzo mojawapo ya kupambana na ugonjwa wa maralia endapo kila mwananchi atazingatia kuvitumia kwa ufanisi.


Mwita amesema kwa mkoa wa Singida kumekua na ongezeko la maambukizi ya Ugonjwa wa maralia kutoka asilimia 0.2 mwaka 2012 hadi kufikia asilimia 5.5 kwa mwaka 2016 licha ya vyandarua 954,644 kugwiwa mkoani hapa kwa mwaka 2016.

Ameongeza kuwa mkakati wa ugawaji vyandarua umelenga kuwafikia asilimia 85 ya watanzania wote ifikapo 2025 na kuutokomeza ugonjwa wa maralia kwa kushirikisha mbinu mbalimbali ikiwemo kupulizia dawa ya ukoka ili kuthibiti mazalia ya mbu pamoja na kuhakikisha matibabu sahihi ya ugonjwa wa maralia yanatolewa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amesema Maralia inakuwepo kutokana na kwamba Mkoa wa Singida sio kame una maji ya kutosha hivyo kusababisha mbu kuzaliana kwa wingi.

Dkt. Nchimbi amesema mikakati iliyopo ni mizuri ila inatakiwa iende sambamba na mikakati mingine ya kupambana na ugonjwa wa maralia kwa kuwa ni ugonjwa ambao hupoteza nguvu kazi ya taifa.


 Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akizungumza katika mkutano wa uelimishaji juu ya mpango endelevu wa ugawaji vyandarau vyenye viuatilifu vya mda mrefu uliofanyika Mkoani Singida.

Wajumbe wa mkutano wa uelimishaji juu ya mpango endelevu wa ugawaji vyandarau vyenye viuatilifu vya mda mrefu uliofanyika Mkoani Singida, wa kwanza ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi Pius Shija Luhende pembeni yake ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida Bravo Lyampembile.


 Maafisa kutoka wizara ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto wakiutambulisha mkoani Singida mpango endelevu wa ugawaji vyandarau vyenye viuatilifu vya mda mrefu.




Mratibu wa ugawaji Vyandarua kutoka Mkoa wa Njombe Mwamaka Assey akieleza uzoefu wake na mbinu bora katika ugawaji wa vyandarua vyenye viuatilifu.

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments