UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki
na Kati, Azam FC, unapenda kuwajulisha wapenzi wa soka nchini kuwa kiungo wa
timu hiyo, Himid Mao ‘Ninja’, amekwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la
kulipwa nchini Denmark.
Himid tayari ameondoka nchini tokea jana
jioni, na atakuwa ndani ya moja ya timu kubwa za nchini humo, Randers FC ambayo
ipo kileleni kwenye Kundi la kwanza ikiwa na pointi 41 kwenye msimamo wa Ligi
Kuu ya Denmark maarufu kama Danish Superliga.
Majaribio ya kiungo huyo yatachukua siku 14
na kwa mujibu wa makubaliano, yatamchukua hadi Mei 15 mwaka huu
yatakapomalizika na kurejea nchini kabla ya shughuli nyingine za makubaliano
kuendelea baina ya timu hizo mbili, endapo watakuwa wamevutiwa na huduma yake.
Azam FC inaamini kuwa Himid Mao atafanikiwa
kwenye majaribio yake hayo kutokana na kiwango kikubwa alichokuwa nacho hivi
sasa na inamtakia kila la kheri katika mtihani aliokuwa nao mbele yake.
Tunaamini kuwa kufaulu kwa Himid kutazidi
kuitangaza Azam FC kimataifa na kufungua milango kwa wachezaji wetu wengine na
Tanzania kwa ujumla kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, ambao hapo baadaye
watakuja kuisaidia vilivyo timu ya Taifa ya Tanzania kutokana na uzoefu mpya
watakaokuwa wameupata huko.
Hii ni mara ya pili kwa Azam FC kutoa mchezaji
wake kwenda kujaribu bahati nje ya nchi ndani ya msimu huu, itakumbukwa kuwa
tayari Desemba mwaka jana imefanikisha safari ya winga wake, Farid Mussa,
kujiunga na Club Deportivo Tenerife inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini
Hispania.
Azam FC itaendelea na utaratibu wake mzuri wa
kutowazuia wachezaji wake kwenda kutafuta bahati za malisho mazuri nje ya nchi,
inaamini kwa kufanya hivyo itakuwa imejitangaza kimataifa, imewasaidia
wachezaji na pia kuusaidia mpira wa Tanzania.
0 Comments