Mwenye kanzu na faili ni muhandisi wa maji Bw Max akikagua bili za LUKU katika kituo cha Manga . |
kituo cha pampu ya maji cha Manga manispaa ya Singida |
Mkuu wa mkoa Dr Nchinbi na mkuu wa wilaya Elias Tarimo wakipozi katika mnada kila jumamosi Manga
|
MIRADI ya visima
kumi katika manispaa ya Singida iliyofadhiliwa na serikali pamoja na benki
ya dunia na kukamilika kwa asilimia mia moja miaka kadhaa iliyopita,hadi sasa
wananchi hawajaanza kunufaika na miradi hiyo.
Hali hiyo kwa kiasi
kikubwa imechangiwa na kamati za maji za miradi hiyo,kutokutambua wajibu
wao.
Pia viongozi wa kisiasa
katika maeneo ya mradi hiyo iliyogharamu fedha nyingi,nao hawaoni tatizo
wananchi wao kukosa maji,ili hali wanayo mradi wa maji uliokamilika.
Hayo yamesemwa mwishoni
mwa wiki na mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Rehema Nchimbi,baada ya kukagua miradi
hiyo, na kujiridhisha kwamba imekamilka na ina thamani ya fedha zilizotumika.
Alisema lengo la miradi
hiyo,ni wananchi wapate maji safi na salama kwa umbali usiozidi kilometa
nne,kama ilivyoagizwa na serikali.
“Katika ukaguzi
wangu,nimebaini mifumo katika miradi hii ya maji,ipo vizuri sana.Baadhi
inaendeshwa kwa umeme na mingine kwa mafuta ya dizel.Makubaliano yalikuwa baada
ya kukamilika miradi hii,iendeshwe na kamati za maji kwa asilimia mia
moja”,alisema.
Akifafanua
zaidi,Dk.Nchimbi alisema wajibu wa kamati hizo,ni pamoja na kukusanya fedha
zinazotokana na kuuza maji kwa wateja.
“Fedha zinazopatikana
ndizo zitakazoendesha mradi husika ikiwemo kugharamia matengenezo ya
mashine,pampu,miundombinu,kununulia dizel,umeme na kumlipa mhudumu wa
mradi.Makubaliano ni miradi ikikamilika,inabaki mikononi mwa wananchi kupitia
kamati zao za maji.Serikali na wafadhili,hawatahusika tena”,amesisitiza.
Aemesisitiza zaidi,kwa
kusema serikali na benki ya dunia imegharamia fedha nyingi kwenye
miradi hiyo,hivyo haiwezi kuendelea kuona miradi inabaki kuwa mapambo,badala ya
kuwaondolea wananchi kero ya maji.
“Naagiza wananchi
wajipange upya chini ya kamati zao,wachague jumuiya za watumiaji maji.Kwenye
jumuiya hizo za maji,wanaweza kuwepo pia wale waliokuwa kwenye kamati za awali
za maji.Jumuiya hizi ziwajibike kikamilifu,zihakikishe zinapata fedha kutoka
mauzo ya maji,ili waendeleshe miradi hiyo kwa ufanisi”,alisema Dk.Nchimbi.
Akiijengea nguvu hoja
yake hiyo,amesema kuanzia mei mwaka huu,anataka kuona kila wananchi
wa manispaa ya Singida,anapata maji safi na salama kwa umbali mfupi.
“Rasilimali maji,ni
msingi kwa maisha ya viumbe hai wakiwemo binadamu.Maji yakiwepo tena kwa umbali
mfupi,mambo yote yatakwenda vizuri.Maji yanasaidia kuweka mazingira safi,na
afya za wananchi zinaboreka.Maji yana mchango mkubwa kwa jamii inayoelekea
kwenye Tanzania ya viwanda”,alisema.
Wakati huo huo,mkuu huyo
wa mkoa,amesema kuwa wanatarajia baadhi ya miradi na hasa ile ya
umeme,kuibinafisha kwenye mamlaka ya maji safi na maji taka (SUWASA),kwa ajili
ya kuiendesha.Mingi itaendelea kumilikiwa na wananchi wenyewe.
Awali ,mhandisi maji
manispaa ya Singida,Max Hassan Kaaya,alisema wanaendelea kuelimisha jamii kuwa
miradi hiyo ya maji,ni mali yao hivyo jukumu la kuiendesha ni lao.Pia wanapaswa
kuilinda na kuitunza vizuri.
Naye mkazi wa kijiji cha
Mtamaa,Hongoa Bunka,alisema elimu zaidi itolewe ili kubadilisha fikiri potofu
ya baadhi ya wananchi kuwa jukumu la kuendesha miradi ya maji ni la
serikali. Wabadilike na kutambua kuwa ni mali yao, na wao ndio watakaoiendesha.
0 Comments