Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli
ametoa onyo kwa vyombo vya habari nchini humo kwa madai vinaandika habari
zisizo za kizalendo.
Kiongozi huyo amemtaka waziri mpya wa Habari Dkt Harrison
Mwakyembe kuvichukulia hatua za kisheria.
"Kila kitu chenye nia ya uchochezi fulani fulani, wao ndio
stori. Sasa Mwakyembe kafanye kazi. Nataka ukafanye kazi. Kama wapo waliokuwepo
waliokuwa wanashindwa kuchukua hatua wewe kachukue," amesema Dkt Magufuli
alipokuwa anamwapisha Dkt Mwakyembe kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo.
Dkt Magufuli pia alimuapisha Prof Palamagamba Aidan John Mwaluko
Kabudi kuwa Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria, na Bw Alphayo Kidata kuwa
Katibu Mkuu wa Ikulu.
"Kwa kuwa wewe ni mwanasheria mzuri, msomi, umesomea mambo
ya habari, kafanye kazi. Serikali ipo. Hatuwezi tukaiacha serikali ikaangamia
kwa sababu ya wat wachache."
"Nchi yetu huko nje ina sifa kubwa sana, juzi tu hapa
amekuja rais wa Benki ya Dunia na amekubali kutupatia Shilingi Trilioni 1.74 na
pia Benki ya Dunia ipo katika mchakato wa kutupatia fedha zingine Shilingi
Trilioni 2.8 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo, haya ndiyo mambo
muhimu ya kuandika lakini hebu angalia siku iliyofuata jinsi magazeti
yalivyoandika," amesema Dkt Magufuli.
0 Comments