RAISI JOHN .P. MAGUFULI YUPO ADDIS ABABA KWENYE KIKAO CHA (AU)



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 29 Januari, 2017 ameanza kuhudhuria mkutano wa 28 wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) unaoendelea Mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.

Asubuhi hii Mhe. Dkt. Magufuli amehudhuria mkutano ulioitishwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Rais wa Jamhuri ya Chad Mhe. Idriss Deby Itno ambapo wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika wanakutana na Katibu Mkuu Mpya wa Umoja wa Mataifa (UN) Mhe. Antonio Guterres.

Madhumuni ya mkutano huo ni kubadilishana mawazo juu ya kuboresha uhusisano kati ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa, hususani katika kuimarisha masuala ya amani na usalama.

Mkutano huo utafuatiwa na mkutano maalum wa wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika utakaoongozwa na Mwenyekiti wa Umoja huo Mhe. Idriss Deby Itno.

Mhe. Rais Magufuli pia atahudhuria chakula cha mchana kilichoandaliwa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika (AUC) Mhe. Dkt. Nkosazana Dlamini Zuma kwa lengo la kutangaza rasmi jina la kituo kipya cha amani na usalama ambacho kimepewa jina la Mwalimu Julius Nyerere ikiwa ni kutambua mchango wake katika kupigania amani na usalama wa Afrika.

Kituo hicho kipo ndani ya majengo ya makao makuu ya Umoja wa Afrika Mjini Addis Ababa na Mhe. Rais Magufuli atatoa hotuba fupi mara baada ya kukitangaza rasmi.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Addis Ababa


29 Januari, 2017

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments