TImu ya Chapecoense ikicheza kabla ya kwenda kwenye fainali |
Ndege iliyokuwa imewabeba watu
81, wakiwemo wachezaji na maafisa wa moja ya klabu kubwa za soka nchini Brazil,
imeanguka ikikaribia mji wa Medellin nchini Colombia na kuua watu 76.
Polisi wamesema watu watano walinusurika lakini watu
wengine wote waliangamia.
Ndege hiyo ya kukodishwa ilikuwa safarini kutoka Brazil
ikipitia Bolivia na ilikuwa imewabeba wachezaji na maafisa wa timu ya
Chapecoense.
Klabu hiyo ilikuwa imepangiwa kucheza mechi ya fainali
ya Copa Sudamericana, dhidi ya timu ya Atletico Nacional ya mji wa Medellin.
Mechi ya awamu ya kwanza ya kombe hilo, la pili kwa
umuhimu Amerika Kusini, ilikuwa imepangiwa kuchezwa Jumatano lakini sasa
imesitishwa.
Timu hiyo inayotoka mji wa Chapeco, kusini mwa Brazil,
ilipandishwa kucheza ligi ya daraja ya kwanza nchini Brazil mwaka 2014 na
ilifika fainali ya kombe hilo la Sudamericana kwa kulaza San Lorenzo ya
Argentina.
Mechi hiyo ilikuwa inatazamwa kama kubwa zaidi katika
historia ya klabu hiyo ndogo.
Shirikisho la Soka la Amerika Kusini (Conmebol) limesema
kwamba limesitisha shughuli zake zote kwa sasa.
Taarifa zinasema ndege hiyo muundo wa British Aerospace
146 ambayo imekuwa ikitumiwa na shirika la ndege la Lamia la Bolivia ilikuwa na
abiria 72 na wahudumu tisa.
Maafisa wa klabu hiyo ya Chapecoense wametoa taarifa
wakisema: "Tunamuomba Mungu awe na wachezaji, maafisa, wanahabari na
wageni wengine watu ambao walikuwa wameandamana na ujumbe wetu."
Wamesema hawatatoa taarifa nyingine hadi ibainike
kiwango kamili cha mkasa huo.
Taarifa zinasema watu wawili kutoka kwa timu hiyo - Alan
Ruschel na Danilo - huenda wamenusurika.
Telemundo Deportes wameandika kwenye Twitter kwamba
Ruschel ameathiriwa na mshtuko lakini ana fahamu na anazungumza. Aidha, ameomba
aruhusiwe kukaa na pete yake ya harusi na awaombe jamaa zake.
0 Comments