WANUSULIKA KIFO BAADA YA KULA CHAPATI SINGIDA



(picha kutoka maktaba yetu)
VIJANA  wawili wakazi wa kijiji cha Mgungira wilaya ya Ikungi mkoani hapa,wamenusurika kifo baada ya kuanza kutapika na kuishiwa nguvu katika shindano la kula chapati 30 pamoja na kunywa vikombe 10 vya chai ya rangi.

Shindano hilo la aina yake kijijini hapo ambalo  ambalo liliandaliwa,kuratibiwa na kudhaminiwa  na Guhumela Lubadila,mshindi alipaswa ale chapati zote 30 na anywe vikombe vyote 10 vya chai ya rangi.Vitu vyote hivyo, gharama yake ni shilingi 9,200.

Kwa mujibu wa afisa mtendaji kata ya Mgungira,Hussein Juma Ng’eni,mshindi wa shindano hilo iliazimiwa asipewe zawadi yo yote,zawadi yake ni chapati 30 na vikombe 10 vya chai atakavyokuwa amekula na kunywa.Shindano hilo,lilifanyika juzi saa tano asubuhi.

Aidha,alisema kuwa endapo vijana hao wakashindwa kufikia lengo la kula chapati 30 na kunywa vikombe vya chai 10,watapaswa wamlipe mmiliki wa mgahawa aliyetambulika kwa jina la mama Benja Mgungira.

Afisa mtendaji kata huyo,alisema  endapo mshindi angepatikana,mdhamini wa shindano hilo,Guhumela,angemlipa mmilikiwa wa mgahawa,shilingi 9,200.

Ng’eni alisema  vijana hao kama igekuwa  ni shindano la mpira wa miguu,wangekuwa wametoka suluhu ya kufungana goli 1-1,lakini wao kila mmoja alikula chapati 19 na vikombe vinne vya chai ya rangi.

“Baada ya kufikia hatua hiyo,kila mmoja alianza kutapika mfululizo huku wakitokwa na jasho jingi na kisha kuishiwa nguvu.Kitendo hicho kilisababisha wakimbizwe katika zahanati ya kijiji,kupatiwa matibabu.Hali zao kwa ujumla,zinaendelea vizuri”,alisema.


Alisema kuwa baada ya kushindwa katika shindano hilo,vijana hao watalazimika kulipa shilingi 9,200 kwa mijubu wa mkataba wa shindalo hilo.

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

1 Comments

  1. Sasa hao jamaa watarudia tena mpambano au ndo mwisho na mwandaaji amekamatwa au hajakamatwa?

    ReplyDelete