Kazi bado ngumu, unaweza kusema hakijaeleweka kuhusiana na suala
la beki Hassan Kessy baada ya Yanga na Simba kukutana leo.
Pande hizo mbili zimekutana bila ya aliyetakiwa kuwa msuluhishi,
Said El Maamry ambaye ni mjumbe wa heshima wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Lakini mwisho, Simba imetaka kulipwa kuanzia kati ya Sh milioni
100 hadi 200 na Yanga wameenda kulijadili.
Taarifa za ndani kutoka katika kikao hicho zimeeleza, kuwa Simba
walianzia Sh milioni 500 wakiondoa dau lao la zaidi ya Sh bilioni moja.
"Kweli, mwisho Simba wamesema wanaweza kulijadili tena
katika ofa kuanzia Sh milioni mia hadi mia mbili.
"Awali Yanga walisema wako tayari kutoa Sh milioni kumi,
lakini Simba wakakataa katakata," kilieleza chanzo.
Katika kikao hicho, Simba iliwakilishwa na Mwenyekiti wa Kamati
ya Usajili, Zacharia Hans Poppe, wakati Yanga iliwakilishwa na mjumbe mmoja wa
kamati ya utendaji, wanasheria wawili na Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit
ambao hata hivyo mara kadhaa walilazimika kutoka nje na kuzungumza na simu.
Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, iliwataka
Simba na Yanga kukutana na kulimaliza suala hilo kabla ya yenyewe kutangaza
uamuzi wake.
0 Comments