TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Mheshimiwa Mhandisi Mathew John Mtigumwe amefanya ziara
katika hospitali ya Wilaya ya Manyoni kukagua huduma zinazotolewa katika
kliniki tembezi ya madaktari bingwa na kuagiza kijana yatima aliyeishi
miaka 16 bila sehemu ya haja kubwa kupatiwa matibabu bila malipo.
Mheshimiwa Mhandisi
Mtigumwe ametoa agizo hilo wakati akitembelea wodi ya wanaume ambapo amekutana
na kijana yatima Mabu Jisinza mwenye umri wa miaka 16 mkazi wa kijiji cha
Mgandu wilayani Manyoni ambaye mara baada ya kuzaliwa bila sehemu ya kutolea
haja kubwa alifanyiwa upasuaji wa kuwekewa njia ya muda sehemu ya tumboni na
baada ya wazazi wake wote kufariki amekosa msaada wa kuwekewa njia ya kudumu.
Mheshimiwa Mhandisi
Mtigumwe amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Daktari John Mwombeki
kuhakikisha anasimamia kijana huyo anapatiwa matibabu stahiki kwakuwa ameishi
kwa kunyanyapaliwa kwa muda wa miaka 16 kutokana na kutoa haja kubwa sehemu ya
tumbo huku akisaidiwa na msamaria mwema Lilema Luhumbika mkazi wa kijiji cha Mgandu
ambaye amekuwa akimpa chakula na malazi.
Aidha Mheshimiwa
Mhandisi Mtigumwe amemuagiza pia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri
ya Manyoni kuchangia fedha endapo kijana huyo atapewa rufaa zaidi na
atakapopona apelekwe shule kwakuwa hajui kusoma, kuandika wala lugha ya
Kiswahili.
Wakati huo huo
Mheshimiwa Mhandisi Mtigumwe ametoa maelekezo kwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya
Manyoni Daktari Fransis Mwanisi kuwa ndani ya mwezi mmoja awe ameanzisha
kliniki ya magonjwa yasioambukiza baada ya kupata maombi kutoka kwa mgonjwa wa
Kisukari Neema Jakson Mbijima aliyeomba kupatiwa huduma ya ushauri kwa wagonjwa
wa kisukari, presha na magonjwa ya moyo.
Mheshimiwa Mhandisi
Mtigumwe ameagiza pia kuongezwa kwa siku za kutolewa huduma hizo za kibingwa
zilizoanza kutolewa wilayani Manyoni siku jumatatu ya tarehe
24 Oktoba na kutarajiwa kukamilika tarehe 28 Oktoba 2016 siku ya ijumaa,
akielekeza kuwa wagonjwa wote watakaoandikishwa mpaka siku ya ijumaa wahudumiwe
wote.
Naye Mganga Mkuu wa
Mkoa wa Singida Daktari John Mwombeki amesema kliniki tembezi ya madaktari
bingwa Wilayani Manyoni inao madaktari bingwa wa macho, meno, watoto, daktari
bingwa wa magonjwa ya akina mama, daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na
daktari bingwa wa upasuaji huku kwa muda wa siku tatu madaktari hao wameona
wagonjwa 1038.
Mheshimiwa Mhandisi
Mtigumwe amezungumza na wagonjwa waliojitokeza kupata huduma hizo na kuwataka
wawataarifu wananchi wengine wajitokeze kwa wingi wasikiapo matangazo ya huduma
za kibingwa kwa kuwa huduma za kibingwa kwa ngazi za wilaya ni nadra kupatikana
na zitawapunguzia gharama na muda wa kufanya kazi za kuzalisha mali, ameongeza
kuwa Mkoa unaweka utaratibu wa kufanya huduma hizo kuwa endelevu.
Huduma za Kliniki
tembezi za madaktari bingwa ukiwa ni utaratibu wa kipekee kufanyika Mkoani
Singida umezinduliwa tarehe 14 Agosti 2016 Wilayani Iramba katika hospitali ya
Kiomboi ambapo jumla ya wagonjwa 1452 walionwa na mwezi Septemba huduma hiyo
imetolewa katika halmashauri ya Wilaya ya Singida ambapo wagonjwa 1064
walinufaikana na sasa ikiwa ni zamu ya halmashauri ya Manyoni ambapo tayari
wagonjwa 1038 wamehudumiwa, utaratibu huu utaendelea mwezi Novemba kwa
halmashauri ya Ikungi.
Imetolewa na;
Grace Gwamagobe
0 Comments