Mke wa Rais wa Nigeria Muhammadu
Buhari, ameonya kuwa huenda asimuunge mkono mumewe kwenye uchaguzi mkuu ujao
iwapo kiongozi huyo hatafanya mabadiliko kwenye serikali yake.
Kwenye mahojiano na BBC, Aisha Buhari amesema rais huyo
"hawafahamu" wengi wa maafisa wakuu aliowateua serikalini.
Amedokeza kwamba serikali imetekwa, na kwamba kuna "watu
wachache" ambao huamua ni nani watateuliwa au kupewa kazi na rais.
Bw Buhari alichaguliwa mwaka jana baada yake kuahidi kukabiliana
na ufisadi uliokuwa umekithiri serikali pamoja na ubaguzi na mapendeleo.
Uamuzi wa mke wa kiongozi huyo kusema hayo hadharani umeshangaza
wengi, lakini ni ishara ya kiwango cha kutoridhishwa kwa watu na uongozi wa
Rais Buhari, anasema mwandishi wa BBC aliyepo Abuja, Naziru Mikailu.
Rais Buhari alitangaza wakati wa kuapishwa kwake kwamba yeye
"hamilikiwi na mtu yeyote na anamilikiwa na watu wote".
Kwenye mahojiano na Naziru Mikailu, Bi Buhari alisema:
"Rais hawafahamu 45 kati ya 50, kwa mfano, kati ya watu aliowateua na mimi
mwenyewe siwafahamu, licha ya kwamba nimekuwa mke wake kwa miaka 27."
0 Comments