Wakati Tanzania leo ikiadhimisha kumbukumbu ya miaka 17
tangu kufariki kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Rais mstaafu wa Awamu
ya Pili, Ali Hassan Mwinyi amesema Taifa limepoteza mwelekeo kwani halina
tena uadilifu aliotujengea Mwalimu Nyerere.
Mwinyi aliyerithi mikoba ya urais kutoka kwa Mwalimu Nyerere
mwaka 1985, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua mdahalo
wa kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na kuzindua kitabu cha 'Selective works of
Mwalimu Nyerere', kilichotafsiriwa na wasomi kutoka China.
Mdahalo huo uliandaliwa na Taasisi ya Uongozi ikishirikiana na
Ubalozi wa China na Asasi ya Urafiki kati ya Tanzania na China. Mwalimu Nyerere
aliyeitawala Tanzania kwa takribani miaka 24, alifariki dunia Oktoba 14, 1999
kwenye Hospitali ya St Thomas jijini London nchini Uingereza ambako alikuwa
akitibiwa maradhi ya saratani ya damu.
Aliiongoza Tanzania kwa uadilifu mkubwa akisimamia misingi ya
haki, umoja, mshikamano, kupiga vita rushwa, kusisitiza kujitegemea na uzalendo
kwa nchi.
“Kazi za kawaida kweli zinafanywa na
zinaendelea, lakini sina uhakika hata kidogo kama uadilifu aliotuachia Mwalimu
bado tunao, sijui nani wa kulaumiwa,” alisema Mwinyi maarufu kama Mzee
Ruksa. Alisema kwa namna ambavyo mambo yanakwenda, ni kiashiria tosha kuwa nchi
haina uadilifu tena.
“Mambo yanavyokwenda kama gari lililo
katika usukani,” alieleza Mwinyi na kuongeza kuwa kuna kila sababu ya kutafakari
hali ilivyo sasa ikilinganishwa na ile ambayo iliachwa na Baba wa Taifa miaka
hiyo 17 toka kufa kwake.
Alisema nafasi hiyo ya mazungumzo katika mdahalo, inawapasa
kukaa kutafakari namna ya kurudisha nchi kwenye reli ambayo iliachwa na Mwalimu
Nyerere ambaye ndiye muasisi wa taifa hili katika misingi ya uongozi.
“Tuna utajiri wa machoni, lakini
ndiyo aliyokusudia Mwalimu? Alitufundisha tuwe matajiri wa vitu au matajiri wa
moyo? Tujali vitu au tujali utu?" Alihoji Rais huyo mstaafu.
Aidha, Mwinyi alisema Mwalimu Nyerere aliijenga nchi kwa misingi
ya utu na kwamba alijitahidi sana kusaidia nchi nyingine za Afrika na hasa zile
za Kusini mwa Afrika kujikomboa ili Afrika yote iwe huru.
Alisema ukombozi huo usiwe wa kuingia msituni kupigana na
kuwatisha akinamama na pia usiwe wa kuwaacha watoto kujilea wenyewe bila
kujengewa misingi ya uadilifu.
“Siku hizi kuna panya road, wametoka
wapi watoto hawa? Sisi wazee hatukuwepo? Au sisi wazee tumetengeneza mazingira
kuwepo hao, mbona mwanzo hawakuwepo sasa wametoka wapi?" Alihoji
tena Mwinyi.
Mwinyi alihoji pia kama mafunzo ya askari yamebadilika, iweje
huko awali askari alikuwa ni mtu ambaye wananchi walikuwa wakimuona
wanamkimbilia tofauti na sasa ambako wananchi wanamkimbia askari.
Aliongeza kuwa pia ni wakati sasa wa kutafakari kwa nini nchi
pamoja na watu wake wamefikia walipo sasa kwani kuna tatizo pia la ubaguzi wa
kikabila katika upatikanaji wa ajira mbalimbali pamoja na ubaguzi wa kidini.
Aidha, alisema kama yatabainika kuwepo mambo hayo, yasiachwe
hivyo badala yake upatikane ufumbuzi ili kurudisha yale yote mema ambayo
yaliachwa na Mwalimu Nyerere katika harakati zake za kuikomboa nchi, uongozi
wake na pia usia wake.
"Baba wa Taifa kwangu alikuwa
zaidi ya kiongozi, alikuwa kaka, rafiki na mtu aliyegeuza maisha yangu na
kunifanya kuwa hivi nilivyo sasa, nimejifunza mambo mengi na nisipoyafuata
itakuwa hasara kwangu,” alisema Mwinyi mmoja wa viongozi wastaafu wanaoheshimika na
kupendwa na Watanzania.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi,
Profesa Joseph Semboja alisema taasisi hiyo inaamini mdahalo huo utazaa maarifa
na kuleta majibu ya changamoto ya karne ya 21.
“Mwalimu leo hii hayupo lakini mawazo
na falsafa zake vinaishi na sisi hivyo ni vyema tuvitumie katika vizazi
vijavyo,” alisema Profesa Semboja.
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku
alisema Mwalimu Nyerere alitujengea misingi ya kujenga taifa katika msingi wa
watu na tabia zao na sio vitu kama vile majengo, madaraja na mengineyo.
Alisema mdahalo ule haukuwa kwa ajili ya kutazama kifo cha
Mwalimu Nyerere, bali kutazama mambo ya msingi ya kulisaidia taifa kusonga
mbele.
Katibu Mkuu wa Asasi ya Urafiki China na Tanzania, Joseph Kahama
alisema nchi mbalimbali za Afrika zimekuwa zikibadili katiba za nchi zao na
viongozi kujiongezea muda wa utawala, lakini nchini mchakato wa Katiba
umedorora kabisa.
0 Comments