MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imepiga marufuku
uingizaji na usambazaji wa simu za mkononi za Smartphone Samsung Galaxy note 7
kwa kuwa zina matatizo ya betri.
TCRA pia imewataka wananchi ambao tayari wanatumia simu hizo
kuzizima na kuzirudisha haraka katika maduka walikozinunua.
Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy, amewataka watanzania
wajihadhari
“Simu hiyo tayari Samsung wenyewe wamesema ina matatizo ya betri
na mara mbili sasa imelipuka,” amesema Mungy.
Amewaomba watu wenye simu za aina hiyo kuzirudisha madukani
haraka wabadilishiwe ama kurudishiwa fedha zao.
“Hata kama uliletewa zawadi kutoka nje ya nchi nawaomba
warudishe huko kuepuka matatizo yanayoweza kujitokeza,” amesema
Mungy.
Hivi karibuni simu aina hiyo iliyothibitishwa na kampuni hiyo
kuwa ilikuwa salama, ilishika moto kwenye ndege nchini Marekani.
Simu hiyo inadaiwa kushika moto ikiwa mikononi mwa abiria
aliyekuwa kwenye shirika la ndege la Southwest Airlines.
Shirika hilo liliwaondoa kwa dharura abiria waliokuwa kwenye
ndege iliyokuwa imepangiwa kusafiri kutoka Louisville, Kentucky, hadi
Baltimore, Maryland muda mfupi kabla ya kupaa.
0 Comments