Taasisi
ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) inashirikiana na Kampuni za
Tukutech Company Ltd kutoka Tanzania, Zanifi Enterprise Ltd kutoka Zambia na
Radai OY kutoka nchini Finland kurusha Ndege Nyuki (Drone) angani kwa ajili ya
kufanya majaribio ya tafiti za miamba na madini katika eneo la Mirerani kwa
kutumia teknolojia ya High Resolution Airborne Geophysical Survey.
Akizunguza katika Semina ya Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Nishati na Madini iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dodoma, Waziri
wa Madini Mhe. Anthony Mavunde alisema, dhamira ya Serikali ni kuona Tanzania
inafanyiwa utafiti wa kina kwa asilimia kubwa ambapo wizara hiyo imekuja na
ajenda ya Vision 2030 "Madini ni Maisha na Utajiri" kwa kufanya
tafiti kwa njia ya Jiofizikia angalau asilimia 50 ifikapo 2030 ambapo kwa sasa
ni asilimia 16 pekee ambayo imefanyiwa utafiti huo.
"GST ni Moyo wa Sekta ya Madini, uwepo wa
taarifa sahihi za kijiolojia ya miamba na madini ndiyo imebeba dhana ya utajiri
wa Tanzania, hivyo niwaombe wajumbe wa Kamati hii tuisaidie GST iwezeshwe kwa
ajili ya maendeleo ya taifa letu," alisema Waziri Mavunde.
Imeelezwa kuwa, awamu ya kwanza ya majaribio ya
tafiti za miamba na madini ilifanyika mwaka jana (2023) katika Mikoa ya Dodoma,
Shinyanga na Geita ambapo awamu ya pili ya utafiti huo unafanyika katika eneo
la Mirerani wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, mkoa wa Lindi pamoja na Mtwara.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Dkt.
Suleiman Serera ameipongeza Wizara ya Madini kupitia GST kwa kutekeleza kwa vitendo
dhana ya Vision 2030 ikiwa ni pamoja na kuratibu zoezi la tafiti ndani na nje
ya ukuta wa Magufuli Mirerani.
"Utafiti wa Madini nchini Tanzania unatoa
mazingira mazuri ya uwekezaji na mazingira mazuri ya uendeshaji katika Sekta ya
Madini, na kuna uwezekano mkubwa wa kugundua maeneo mapya kwani maeneo mengi
bado hayajafanyiwa utafiti wa kutosha," amesema Dkt. Serera.
Akizungumza katika eneo la Utafiti, Kaimu
Mkurugenzi wa Kanzidata ya Taifa ya Rasilimali Madini Bi. Hafsa Maulid amesema
GST imejipanga kikamilifu kutekeleza kwa vitendo dhana ya Vision 2030 kwa
kufanya tafiti za kina kwa njia ya Jiofizikia angalau asilimia 50 ifikapo 2030
kama ajenda ya wizara inavyosema ambapo kwa sasa ni asilimia 16 pekee ambayo
imefanyiwa utafiti huo.
GST itaendekea kushirikiana na taasisi nyingine za
utafiti ili kutengenezea kanzidata ya taarifa sahihi za kijiolojia kwa ajili ya
maendeleo ya taifa.
0 Comments