SAUTI YA WARIOBA: “SERIKALI IMETUPA NGUVU KUBORESHA HUDUMA ZA MAJI”

 




Singida

Mamlaka ya Wasilimali za Maji Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Singida imeendelea kufanya vizuri katika utekelezaji wa miradi ya maji vijijini, ambapo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imepokea zaidi ya shilingi bilioni 35 kwa ajili ya miradi hiyo katika wilaya tano za mkoa huo.

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Singida, Mhandisi Lucas Saidi, amesema hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake mjini Singida, na kueleza kuwa mafanikio hayo yametokana na usimamizi mzuri wa serikali pamoja na ushirikiano wa wananchi.

“Tokea Januari 2021 tulikuwa na wastani wa asilimia 57 ya upatikanaji wa maji vijijini, lakini kufikia Juni 2025 tumefikia asilimia 71.3. Hii ni hatua kubwa inayodhihirisha dhamira ya serikali ya kuwahudumia wananchi,” amesema Mhandisi Saidi.

Ameongeza kuwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026, RUWASA imetenga zaidi ya shilingi bilioni 11.6 kwa ajili ya kutekeleza miradi mipya ya maji vijijini, ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za serikali ya awamu ya sita katika kuboresha huduma za maji safi na salama.

Hata hivyo, amesema changamoto kubwa inayojitokeza ni hali ya ukame na upatikanaji mdogo wa maji ardhini kutokana na jiografia ya ukanda wa kati, hali inayosababisha visima kuchimbwa kwa kina kirefu zaidi.

Mhandisi Saidi ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutunza miundombinu ya maji inayowekwa na serikali ili miradi hiyo iwe endelevu na iwanufaishe kwa muda mrefu.

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments