NEC YATOA KIBALI KWA TANLAP KUTOA ELIMU YA MPIGA KURA NCHINI

 


SINGIDA

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa kibali kwa Shirika la Mtandao wa Mashirika ya Wasaidizi wa Kisheria Nchini (TANLAP) kutoa elimu ya mpiga kura katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu taratibu za kupiga kura kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Msaidizi wa kisheria kutoka TANLAP mkoani Singida, Theresia Mande, akizungumza na wananchi katika Soko Kuu la Kimataifa la Vitunguu Singida, amewahimiza wananchi kuzingatia taratibu zote zilizowekwa na NEC, ikiwemo kuhakikisha kila mtu anapiga kura katika kituo alichojiandikishia.

Aidha, Mande amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi na kwa wakati siku ya uchaguzi ili kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura.

“Kwa mwaka huu, Tume imeweka utaratibu utakaowawezesha wafungwa kushiriki kupiga kura ya urais pekee, ambapo vituo vya magereza vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 9:00 alasiri, huku vituo vingine vilivyopo uraiani vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni,” amesema Mande.

Ameongeza kuwa kupiga kura ni haki ya msingi ya kila raia mwenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea, huku akisisitiza umuhimu wa kutoa kipaumbele kwa wazee, kina mama wajawazito, wenye watoto wachanga, pamoja na watu wenye ulemavu watakaofika vituoni.

Elimu hiyo imeendelea kutolewa katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu kama masokoni, vituo vya mabasi na maeneo ya wazi, lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu utaratibu wa uchaguzi na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kidemokrasia.



Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments