MAENDELEO YA SEKTA YA MAWASILIANO NA VIWANDA KUBORESHA MAISHA YA WANANCHI MKOANI SINGIDA


Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe,Jerry Silaa akiwasili katika Mradi wa shule ya sekondary ya Sekotoure wilaya ya Singida.








 Singida

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb.) ametembelea na kukagua miradi ya viwanda inayojengwa Mkoani Singida, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya uchumi wa viwanda yenye lengo la kupunguza umaskini na kukuza pato la Taifa. Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na mradi wa kiwanda cha Taifa Gas na kiwanda cha mafuta ya kupikia cha Wild Flower & Oil Mills Co. Ltd.

Akiendelea na ziara yake Mkoani Singida tarehe 25 Oktoba 2024, Waziri Silaa alionesha kuridhishwa na maendeleo ya mradi wa kiwanda cha Taifa Gas, ambao unachangia utekelezaji wa mkakati wa kitaifa ulioanzishwa na Rais Samia wa kuhakikisha nchi nzima inatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Aidha, Waziri Silaa alitembelea ujenzi wa kiwanda cha Wild Flower & Oil Mills Co. Ltd, ambacho kinatarajiwa kuzalisha mafuta ya alizeti. Ujenzi wa kiwanda hiki umefikia asilimia 95 na unatarajiwa kutoa ajira 190 za moja kwa moja na 460 zisizo za moja kwa moja, na hivyo kunufaisha wakulima wa alizeti takribani 26,000.

Mbali na miradi ya sekta ya viwanda, Waziri Silaa alizindua mnara wa mawasiliano wa kampuni ya simu ya Airtel katika kijiji cha Mikuyu, uliogharimu shilingi milioni 115 kwa msaada wa Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF). Mradi huu ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuwaunganisha Watanzania wote na huduma za kidijitali.

Kabla ya kumaliza ziara yake, Waziri Silaa alizungumza na wananchi wa kijiji cha Makuro na kuwasisitizia umuhimu wa miradi hii katika kuboresha hali ya maisha ya jamii. Pia alikagua mradi wa majitaka utakaosaidia kuboresha usafi wa mazingira na kusaidia shughuli za kilimo.

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments