BAKWATA MKOA WA SINGIDA YATOA TAMKO KWA VIJANA


BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Singida limekemea vikali tabia iliyojengeka kwa baadhi ya vijana wa kiume na wa kike ya kuvaa mavazi ya kuiga na yasiyompendeza Mungu na kuwataka wazazi na walezi wa vijana hao kuwajengea mazingira mazuri vijana wao ya kuwa na nidhamu.

Akifungua maulidi ya Jumuiya ya akina mama (JUWAKITA) Mkoa wa Singida,Katibu wa Bakwata Mkoa wa Singida,Alhaji Buruhani Mlau amesema wakati umefika kwa vijana kudumisha utamaduni uliokuwepo awali na kuondokana na tabia ya  kuvaa mavazi ya kuiga na yasiyofaa.

Hata hivyo Alhaji Mlau ametumia fursa hiyo pia kuwataka  waumini wa madhehebu ya dini ya kiislamu kujitambua, kubadilika na kisha waache mazoea na waondokane na mioyo ya ubinafsi kwani endapo wataendelea kuwa na mioyo ya ubinafsi wao ndiyo watakaoumia.

Kwa upande wake Mjumbe wa Baraza la UWT Taifa Mkoa wa Singida,Bi Diana Chilolo akizungumza na akina mama wa jumuiya hiyo ya kiislamu amewahimiza kusoma korani tukufu na kwamba endapo watasoma kikamilifu maandiko hayo matakatifu watakuwa akina mama bora katika ndoa zao na pia wazazi bora.

Awali akisoma risala fupi ya JUWAKITA,Katibu wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Singida,Bi Adija Omari amesema kwamba lengo la kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ni kuwahamasisha wanawake wa kiislamu,hasa vijana kujitambua na kuelewa mazingira ya kijamii,kisiasa na kiuchumi ili waweze kufahamu vizuri changamoto na fursa zilizopo mbele yao.

Hata hivyo Bi Adija ameyataja mafanikio yaliyopatikana kutokana na jumuiya hiyo kuwa ni pamoja na kutoa ushauri nasaha kwa vijana wa kike na akina mama kuhusiana na madhara ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (HIV),ndoa za utotoni,ndoa za jinsia moja,mirathi pamoja na talaka.


Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments