MKUU WA WILAYA SINGIDA AWAPONGEZA WATUMISHI NA WAKULIMA BORA WA MWAKA 2025/2026

 

Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhe Godwin Gondwe akiongea katika uzinduzi wa msimu wa Kilimo katika kata ya Mtinko.

Bi Ester Chaula akipokea tuzo maalum ya utendaji bora kutoka kwa DC Gondwe.

          Afisa kilimo na Uvuvi Bi Natalia Mosha akipokea tuzo kutoka kwa Dc Gondwe.





SINGIDA

Na Mwandishi Wetu

Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Wilaya ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhe. Godwin Gondwe, ameongoza uzinduzi rasmi wa msimu mpya wa kilimo wa mwaka 2025/2026, katika hafla iliyofanyika leo Oktoba 22, 2025, katika kijiji cha Mtinko, kata ya Mtinko, Halmashauri ya Wilaya ya Singida.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, wataalamu wa kilimo pamoja na wananchi na wadau mbalimbali wa sekta hiyo.

Akihutubia katika hafla hiyo, Mhe. Gondwe ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa wananchi, akisema kuwa hatua hiyo ni ya kipekee na ya kupongezwa.

“Natamani watanzania watambue kuwa si jambo la kawaida katika nchi nyingi za Afrika kuona Serikali inatoa ruzuku kwa wakulima. Leo tunashuhudia wenyewe namna ambavyo mfumo huu umeinufaisha sekta ya kilimo. Wafanyabiashara wa mbegu na mbolea wanasema wazi kuwa biashara zao zimeimarika baada ya kuingia kwenye mfumo wa ruzuku. Tanzania sasa imeingia kwenye ramani ya dunia kwa kumuwezesha mkulima — hili si jambo dogo,” alisema Mhe. Gondwe.

Katika hatua nyingine, Mhe. Gondwe alikabidhi vyeti vya pongezi kwa watumishi wa idara ya kilimo waliofanya kazi bora, pamoja na wakulima waliofanya vizuri katika shughuli zao. Pia, tuzo maalum zilitolewa kwa Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, na Mkuu wa Idara ya Kilimo kwa kutambua mchango wao katika mafanikio ya sekta hiyo ndani ya Halmashauri.

Aidha, kupitia hafla hiyo, Mhe. Gondwe aliongoza wananchi kutembelea mabanda ya wadau wa kilimo ambapo walijionea pembejeo mbalimbali kama mbegu, mbolea, viuatilifu, na vifaa vya kisasa vya kilimo vikiwemo matrekta. Hafla hiyo ilitoa fursa kwa wakulima kujifunza mbinu na teknolojia mpya kupitia wataalamu na wadau wa kilimo waliokuwa wakitoa elimu na mafunzo.

 

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments