Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harisson
Mwakyembe (Mb) ametangaza rasmi kanuni mbili za Sheria ya Mawasiliano ya
Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya Sura namba 306 ya mwaka 2010, katika gazeti
la Serikali namba 133 (GN.No.133) na 134 (GN.No.134) zilizochapishwa tarehe
16/03/2018.
Kanuni za Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta
(Maudhui ya Habari za Mtandaoni) ya mwaka 2018 ijulikanayo kama The
Electronic and Postal Communications (Online Content) Regulations, 2018 zimetangazwa
kupitia Tangazo la Serikali Namba 133 (GN.No.133).
Kanuni nyingine ni Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na
Posta (Maudhui ya Utangazaji katika Redio na Runinga) ya mwaka 2018 ijulikanayo
kama The Electronic and Postal Communications (Radio and Television
Broadcasting Content) Regulations, 2018 ambazo zimetangazwa kupitia tangazo
la Serikali namba 134 (GN.No.134).
Kanuni hizi kwa pamoja zimetengenezwa chini ya Kifungu cha 103
cha sheria ya EPOCA na zimetiwa saini na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe ambaye ndiye mwenye dhamana na Maudhui ya
Habari na Utangazaji.
Kwa ujumla kanuni hizi zinalenga kuongeza ufafanuzi wa mambo
muhimu katika Sekta ya Habari, kwa ajili ya kuongoza vyombo vyenye mamlaka ya
kusimamia pamoja na kurahisisha utekelezaji kwa watumiaji mbalimbali wa huduma
ya Sekta hiyo.
Mchakato wa kuandaa Kanuni hizi ulihusisha wadau mbalimbali wa
Habari wakiwamo wamiliki wa vyombo, watoa huduma za mawasiliano ya mtandaoni,
watumiaji wa mtandao, waandishi wa habari, pamoja na wanaharakati na watetezi
wa haki za walaji wa huduma za sekta hii pamoja na Wizara ikisaidiana na
wataalamu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Kanuni za Maudhui ya Utangazaji wa kwenye redio na kwenye
runinga pamoja na mambo mengine zimefafanua juu ya dhana kuu mbili ambazo
zimekuwa katika mijadala ya watoa huduma na watumiaji wengi, mambo hayo ni
kuhusu Chaneli ambazo ni lazima kubebwa na anayemiliki miundombinu ya kurushia
matangazo hata kama hazijalipiwa kwenye king’amuzi cha mlaji wa mwisho ( free
to air channels).
Aidha, Kanuni zinawaelekeza wamiliki wa mitambo ya kurushia
matangazo kulazimika kurusha hewani Chaneli ya umma (must carry public
broadcaster channel) pasipo chombo cha umma kinachorusha chaneli hiyo au
mwananchi anayemiliki king’amuzi kulipia chochote.
Vilevile Kanuni hizo zimeeleza juu ya taratibu za utoaji wa
leseni za maudhui kwa vyombo vya habari, aina za leseni, masharti ya utoaji wa
maudhui kwa vyombo vya habari, masharti ya urushaji vipindi, masharti ya jumla kwa
leseni za huduma za maudhui.
Pia, Kanuni hizo zimeeleza juu ya viwango vya kitaalamu na
kiufundi katika huduma za utangazaji, utoaji wa vibali vya ujenzi wa
miundombinu ya utangazaji, aina za huduma na leseni za maudhui, wajibu wa vituo
vya umma, wajibu wa vituo vya kibiashara, wajibu wa vituo vya kijamii, wajibu
kwa utangazaji wa maudhui yanayolipiwa pamoja na masharti kwa kampuni za
miundombinu ya maudhui.
Kanuni hizi pia zimezingatia kuwalinda watoto dhidi ya maudhui
yasiyofaa, muda kwa vipindi ambavyo watoto hawaruhusiwi kuona kama vile
utangazaji wa maudhui yenye vitendo vya ngono au maudhui yanayoonesha vurugu.
Mambo mengine ni masharti ya kutangaza mwenendo wa Mahakama au
Bunge, masuala ya uchaguzi, masharti ya kutangaza maudhui kwa watu wenye mahitaji
maalum, masharti kwa utangazaji wa vipindi vya mahojiano, lugha ya kutumia
katika utangazaji.
Zimeelezea pia juu ya utangazaji wa maudhui ya ndani ya nchi na
vipindi vyenye maslahi ya Kitaifa, vipindi vya taarifa za kiuchunguzi au
masuala ya watu binafsi (Faragha), Utangazaji wa vipindi vya moja kwa moja.
Vilevile kumewekwa utaratibu wa kupokea na kusikiliza malalamiko
ya walioathiriwa na habari za mtandaoni pamoja na adhabu kwa wanaofanya makosa
kupitia mawasiliano ya mtandaoni.
Kanuni hizi zitafanya kazi chini ya Kamati ya Maudhui ambayo
nayo imeundwa chini ya Sheria hiyo. Wadau mbalimbali wa vyombo vya habari na
utangazaji pamoja na watumiaji wa mawasiliano ya habari kwa njia ya mtandao
wanashauriwa kuzipitia kanuni hizo na kuzisoma kwa kina ili kuelewa mambo
yaliyofafanuliwa.
Kanuni hizi zinapatikana katika
Tovuti ya Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na
Michezo (www.habari.go.tz) kisha ingia sehemu ya machapisho bofya kipengele cha Sera,
sheria na kanuni, pia waweza kutembelea tovuti ya TCRA (




0 Comments