Na Grace gwamagebe
Halmashauri saba za Mkoa wa Singida zimeagizwa kununua vitanda
kumi kwa ajili ya akina mama kujifungulia ili kuunga mkono juhudi za Rais wa
Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli za kuboresha afya ya
mama na mtoto.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi ametoa agizo hilo
mapema leo katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida mara baada ya kupokea
vitanda vya kujifungulia 14, magodoro 20 na mashuka 50 vyenye thamani ya zaidi
ya milioni 121 kutoka kwa Rais Magufuli.
Dkt Nchimbi amesema halmashauri zinatakiwa kuiga mfano wa Rais
Magufuli anayojali afya kwa ajili ya wananchi hivyo wanapaswa kutenga kiasi cha
shilingi milioni kumi na tatu kwa ajili ya kununua vitanda hivyo kwa mwaka huu
wa fedha.
“Tumezoea kupokea tu na tumepokea sana vifaa tiba kutoka kwa
rais wetu mpendwa Magufuli, hebu tujifunze upendo wake kwa wananchi, hivyo
naagiza kila halmashauri inunue vitanda kumi vya kujifungulia nadani ya mwaka
huu wa fedha”, amesisitiza Dkt Nchimbi.
Amengeza kuwa akina mama wajawazito wanatakiwa kujifungulia
katika vituo vya kutolea huduma za afya kwakuwa kuna huduma bora zaidi huku
akiwataka wakunga wa jadi wawasaidie wajawazito kufika katika vituo hivyo.
Aidha Dkt Nchimbi amemshukuru Mbunge wa Viti Maalumu Singida
Aisharose Mattembe aliaminiwa na Rais Magufuli na kumtuma kufikisha vitanda
hivyo Mkoani Singida huku akimtaka kuanzisha tunzo ya wakunga watakaosaidia
kufikisha akina mama wajawazito katika vituo vya kutolea huduma za afya.
“Natoa shukrani zangu za dhati kwa niaba ya wananchi wa Singida
kwa Rais Magufuli kwa kuendelea kutujali wana Singida, pia nakushukuru kwa
uaminifu wako mbuge wetu Mattembe kwa kufikisha vifaa hivi salama ila naomba
uanzisishe tunzo ya wakunga wa jadi watakaowashauri vizuri na kuwafikisha
katika vituo vya kutolea huduma za afya akina mama wajawazito”, amesema Dkt
Nchimbi.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Emmanuel
Kimario amemshukuru Rais Magufuli kwa vitanda hivyo vitakavyosaidia kupunguza
uhaba wa vitanda, hasa kwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa ambapo wajawazito wengi
wanapenda kujifungulia kwakuwa na imani napo kutokana huduma bora zinazotolewa.
Dkt Kimario amesema mpaka sasa bado kuna akina mama
wanajifungulia nyumbani na kwa wakunga wa jadi jambo linalohatarisha afya ya
mama na motto hivyo wafuate ushauri wa kufika katika vituo hivyo mara tu wanapo
hisi kuwa na ujauzito.
‘Takwimu za kuanzia kipindi cha mwezi wa saba mpaka wa tisa
mwaka huu zinaonyesha kuwa akina mama waliojifungulia ni 12,431 ambapo kati yao
190 wamejifunguliwa nyumbani, akina mama 78 wamejifunguliwa kwa wakunga
na wengine 258 wamejifungulia njiani”, amesema Dkt Kimario.
Kwa upande wake Naibu Meya wa Manispaa ya Singida Yagi Maulidi
Kiaratu amewapongeza wauguzi na madaktari wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa
huduma nzuri wanazotoa hadi kusababisha wagonjwa wengi kukimbilia hapo.
Amesema, “unakuta mgonjwa anaacha aspirini pale kituo cha afya
Sokoine na kuja hapa Hospitali ya Mkoa akiwa na imani kubwa hata akipewa dawa
ile ile hapa atapata nafuu, hivyo nawapongeza sana na muendelee na moyo huo wa
kuwahudumia vizuri wagonjwa hata kama tunapata changamoto akati wa kuwalaza
wanapokuwa wengi”, amesisitiza Kiaratu.
Ameongeza kuwa Mbunge wa Viti maalumu Singida Aisharose Mattembe
amekuwa mstari wa mbele katika kusimamia afya ya mama na mtoto inaboreka Mkoani
Singida huku akijitolea vifaa mbalimbali kama vitanda na mashuka, jambo
ambalo ni faraja kwa akina mama na wananchi wote.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akifungua moja
kati ya vitanda 14 vya kujifungulia vilivyotolewa na Rais Magufuli mapema leo
katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida.
Wauguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida wakifurahia
mara baada ya kukabidhiwa vitanda vya kujifungulia vilivyotolewa na Rais
Magufuli.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Emmanuel
Kimario akimshukuru Rais Magufuli kwa kuwapatia vitanda vya kujifungulia ili
kupunguza uhaba wa vitanda kwa Mkoa was Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akisaidiana na
wataalamu wa afya pamoja na Mbunge wa Viti maalumu Aisharose Mattembe kufunga
moja kati ya vitanda 14 vya kujifungulia vilivyotolewa na Rais Magufuli mapema
leo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida.
0 Comments