"IKUNGI ELIMU CUP 2017" SINGIDA



Mkuuwa wilaya ya Ikungi Mh Miraji Mtaturu akiongea katika uzinduzi huo uliyofanyika katika viwanja vya  shule ya sekondari ya Ikungi.

Na Grace gwamagobe ofisi ya mkuu wa mkoa Singida

Wanasiasa hasa wasomi na wale wenye ushawishi mkubwa wametakiwa kuacha kulalamika na kutoa kauli ambazo hazitawasaidia wananchi katika kuwatatulia matatizo na kero zao bali waungane na serikali katika juhudi zinazoonekana za kuleta maendeleo.

Rai hiyo imetolea na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu jana wakati wa uzinduzi wa Ligi ya mpira wa miguu ambayo ina lengo la kuutambulisha kwa wananchi na wadau mbalimbali mfuko wa elimu wa wilaya hiyo ili wahamasike kuuchangia.

Mtaturu amesema baadhi ya wanasiasa maarufu wamekuwa wakitumia muda mwingi kueleza matatizo na kero za wananchi bila ya kuonyesha suluhisho au kusaidia kutatua kero hizo jambo ambalo halimsaidii mwananchi kwa namna yoyote.

“Baadhi ya Wanasiasa utawaona mstari wa mbele kutajataja kero za wananchi wanapokuwa majukwaani wakati hawatoi mchango wowote wa kutatua kero hizo au hata kueleza mapendekezo ya nini kifanyike, acheni kufanya hivyo kwakuwa mna watonesha vidonda wananchi, kusema sema hakusaidii, onyesha njia ya kumsaidia mwananchi kama ambavyo sisi tunafanya leo katika sekta ya elimu”, amesema Mtaturu. 

Amesema Sekta ya elimu Wilayani humo inakabiliwa na uhaba wa nyumba za walimu, vyumba vya madarasa na maabara ambapo mfuko wa elimu una mpango wa miaka mitatu yaani 2017-2020 wa kukusanya zaidi ya bilioni tatu zinazohitajika kutatua changamoto hizo. 

Mtaturu amesema kati ya mahitaji ya maabara 90 wilayani humo, zipo maabara nne tu na kwa kuanzia mfuko huo umeweka malengo ya kuhamasisha wananchi kufyatua tofali elfu kumi kwa kila kata ili ziweze kutatua changamoto hiyo.

Ameongeza kwa kuwapongeza wananchi, viongozi na madiwani waliojitokeza kuchangia mfuko huo ambapo yeye amechangia mifuko mia moja ya simenti, wadau na wananchi walitoa mifuko 194 ya simenti, fedha taslimu laki nane, ahadi milioni moja laki tisa, mchanga ‘trip’ tano na moramu.

“Nawashukuru sana madiwani wa Ikungi na wananchi kwakweli tumeanza vizuri na nina imani mfuko huu wa elimu utasaidia kupunguza changamoto za sekta ya elimu wilayani humu, tunaendelea kukaribisha wadau mbalimbali, lakini pia wananchi msisite kama una mchanga leta, una siment hata maji tu ni mchango pia tusikariri mchango lazima ni fedha”, ameongeza.


Mgeni rasmi wa ufunguzi wa Ligi hiyo Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt Angelina Mageni Lutambi aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amewapongeza wananchi wa Ikungi kwa kuupokea mfuko huo kwa hamasa kubwa.

Dkt Lutambi amesema mfuko huo utaboresha elimu hasa ujenzi wa maabara ambazo ni msingi wa maendeleo ya sayansi ambapo bila kufanya vizuri katika sayansi wilaya hiyo haitaweza kujikomboa katika viwanda na kuelekea uchumi wa kati.

“Ukombozi wa nchi yoyote bila sayansi haiwezekani, Ikungi mkiboresha mazingira ya hawa wana sayansi wanafunzi mnatengeneza jamii ya wanasayansi ambao wataikomboa wilaya yetu kwa kuweka ubunifu kwenye viwanda ambavyo hukuza uchumi kwa haraka”, amesisitiza.

Ameongeza kuwa Ligi hiyo isaidie kuwaunganisha wananchi hao na kuchangamkia katika kuchangia maendeleo ya elimu wilayani humo, aidha ameitaka halmashauri kusimamia mfuko huo kwa umakini ili uweze kutekeleza majukumu yaliyotarajiwa.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ACP Debora Daudi Magiligimba amesema michezo huleta amani na kusaidia katika kuhamasisha maendeleo hivyo basi ligi hiyo isaidie kuhamasisha kwa amani uchangiaji wa mfuko huo.

Wakati huo huo ACP Magiligimba amewapongeza wananchi wa Ikungi na Mkoa wa Singida kwa kushirikiana na jeshi la polisi katika kupunguza wahalifu na uhalifu.

Amesema uhalifu umepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na ushirikiano wanaoupata kutoka kwa wananchi licha ya uhalifu wa ubakaji ukionekana kuongezeka hivyo amewataka wananchi kuendela kutoa ushirikiano ili ubakaji uishe.

ACP Magiligimba amewataka wananfunzi kuacha vitendo vya ngono na vijana kuacha matumizi ya madawa ya kulevya kwakuwa yote hayo huharibu maisha yao bali wakazane katika masomo na michezo.

Ligi ya mpira wa miguu Wilayani Ikungi yenye lengo la kuhamasisha wananchi na wadau kuchangia mfuko wa elimu imeanza rasmi jana na inatarajiwa kuhitimishwa mwezi Septemba ambapo zaidi ya timu 69 zitashiriki.



 Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu akiwania mpira katika mechi ya ufunguzi wa Ligi ya elimu yenye lengo la kutunisha mfuko wa elimu wilayani humo, mechi kati ya madiwani wa Halmashauri ya Ikungi na Manispaa ya Singida ilizindua ligi hiyo na kutoka sare ya bila bila.

 Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt Angelina Mageni Lutambi akifyatua tofali wakati wa uzinduzi wa Ligi ya elimu yenye lengo la kutunisha mfuko wa elimu wilayani humo, Matofali elfu kumi yanatarajiwa kufyatuliwa kwa kila kata.

 Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu akifyatua tofali wakati wa uzinduzi wa Ligi ya elimu yenye lengo la kutunisha mfuko wa elimu wilayani humo, Matofali elfu kumi yanatarajiwa kufyatuliwa kwa kila kata.

 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ACP Debora Magiligimba akizungumza wakati wa uzinduzi wa Ligi ya elimu yenye lengo la kutunisha mfuko wa elimu wilayani humo, Matofali elfu kumi yanatarajiwa kufyatuliwa kwa kila kata.

Sehemu ya mchango ya simenti kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu pamoja na wadau mbalimbali ambapo Matofali elfu kumi yanatarajiwa kufyatuliwa kwa kila kata ili kutunisha mfuko wa elimu Wilayani humo wenye lengo la kutatua baadhi ya changamoto ya ukosefu wa maabara na vyumba vya madarasa. 

 Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt Angelina Mageni Lutambi akimkabidhi bahasha yenye shilingi laki mmoja kati ya wanafunzi 16 wa Sekondari ya Ikungi waliopata ufaulu wa daraja la kwanza katika matokeo ya kidato cha sita kama sehemu ya kuhamasisha wanafunzi na walimu kufanya vizuri, aidha wanafunzi hao  walipatiwa shilingi laki moja kila mmoja huku walimu wakipatiwa motisha ya shilingi milioni moja.

Baadhi ya wananchi wakijitolea kufyatua tofali ambapo Matofali elfu kumi yanatarajiwa kufyatuliwa kwa kila kata ili kutunisha mfuko wa elimu Wilayani humo wenye lengo la kutatua baadhi ya changamoto ya ukosefu wa maabara na vyumba vya madarasa.

Tuandikie Maoni Yako Hapa

Post a Comment

0 Comments