Na,Jumbe Ismailly
IGUNGA
WAKAZI watatu wa mjini Igunga wanashikiliwa na polisi wilayani
Igunga,Mkoani Tabora kwa tuhuma za kukutwa na madawa ya kulevya aina ya Heroin.
Walioshikiliwa na jeshi hilo kutokana na tuhuma hizo kuwa ni
pamoja na Mohamedi Hamisi (34) mkazi wa mtaa wa Mwayunge,aliyekutwa akiwa na
kete 7 za madawa hayo ya kulevya aina ya Heroin,Steveni Mtani(39),mkazi wa mtaa
wa stoo aliyekamatwa na kete tano za madawa ya kulevya aina ya Heroin na Mussa
Salum (37) mkazi wa mtaa wa Mwayunge ambaye alikamatwa na gramu 2 za madawa ya
kulevya aina ya Heroin.
Akithibitisha kukamatwa kwa watu hao,Mwenyekiti wa serikali ya
Mtaa wa Mwayunge,kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA ) Bwana
Abeli Shampinga amesema polisi kwa kushirikiana na yeye walimkamata Mohamedi
Hamisi saa 12:30 alfajiri akiwa na kete 7 akiwa amezificha kwenye mfuko
wa plastiki,au maarufu kwa jina rambo huku akiwa amezihifadhi kwenye sinki la
choo katika nyumba anayoishi.
Mwenyekiti huyo hata hivyo ametumia fursa ya zoezi hilo
kulipongeza jeshi la polisi kwa kazi nzuri ya kufanikisha kukamatwa kwa madawa
hayo ambayo yamekuwa yakiharibu maisha ya vijana huku akiwataka wananchi kuunga
mkono juhudi za Rais Magufuli za kuwafichua wauzaji pamoja na watumiaji ili
waweze kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Hata hivyo kwa upande wake Kamanda wa polisi Mkoa wa
Tabora,Kamishna Msaidizi wa polisi, Willbroad Mtafungwa amethibitisha
kukamatwa kwa vijana hao,julai,22,mwaka huu saa 12:30 alfajiri katika Mtaa wa
Mwayunge,kata ya Igunga mjini wakiwa na madawa hayo ya kulevya aina ya Heroin.
Kamanda Mtafungwa hata hivyo aliweka bayana kwamba watuhumiwa
wote watatu wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani Julai,24 mwaka huu na kutoa onyo
kali kwa wale wote wanaojihusisha na uuzaji na utumiaji wa madawa ya
kulevya kuacha mara moja.
Kwa mujibu wa Kamanda Mtafungwa jeshi la polisi Mkoa wa Tabora
linaendelea na operesheni ya kuwasaka katika wilaya zake zote wanaojihusisha na
tabia hiyo.
0 Comments