KITUO cha Afya cha tarafa ya Kintinku,wilayani Manyoni,Mkoani
Singida kinakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo miundombinu chakavu ya
majengo ya wodi za akinama na watoto wadogo,huduma ya maji,madawa na vifaa tiba
hali inayochangia kituo hicho kutoa huduma chini ya kiwango.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha afya Kintiku,Bwana Limbu Mundika
ameyasema hayo alipokuwa akiwaelezea waandishi wa habari waliokwenda kutembelea
kituo hicho cha afya baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi kuwa
kinakabiliwa na changamoto mbali mbali zinazokwamisha utoaji wa huduma stahiki.
Aidha Mganga mfawidhi huyo amezitaja baadhi ya changamoto
zilizopo katika Kituo hicho kuwa ni shida ya maji katika eneo hilo kwani
wamekuwa wakilazizmika kuyafuata umbali wa kati ya kilomita nne hadi tano na
uchakavu wa miundombinu.
Kwa mujibu wa Bwana Mudinka licha ya eneo la kutoa huduma ni
vijiji vitatu ambavyo ni Kintinku,Udimaa na Lusilile lakini kutokana na kwamba
wapo mpakani,vile vile wanahudumia watu kutoka wilaya ya Bahi,Chemba na vijiji
jirani vinavyozunguka tarafa hiyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya
Manyoni,Bwana Charles Fussi licha ya kukiri changamoto zilizopo kuwa ndizo
zinazokwamisha utoaji wa huduma kwa ufanisi,lakini hata hivyo amesema hakuna
mpango ulioandaliwa na Halmashauri hiyo wa kukarabati majengo hayo zaidi ya
msaada utakaotolewa na TAMISEMI ambao wameahidi kujenga majengo saba mapya
katika Kituo hicho cha afya.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kintinku,Bwama Gasper Mgante
amebainisha kuwa wodi ya wazazi ilianza kupasuka na kuwa na nyufa nyingi katika
kipindi cha kuanzia mwaka 2015 na 2016 na hatimaye jengo hilo la kujifungulia
akina mama pamoja na kupumzika likaonekana kuwa halifai kuendelea kutumika.
0 Comments